Wednesday, January 9, 2013

Pigo jingine kwa Waandishi, Mwandishi anyongwa na kupigwa Risasi

Mwandishi wa Habari na Mtangazaji wa Kituo cha Redio Kwizera, Wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, Issa Ngumba ameuawa  na watu wasiojulikana.

Tukio hili la kusikitisha, limetokea juzi wilayani humo baada ya mwandishi huyo kupotea kwa siku tatu.
Habari kutoka wilayani Kibondo zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa porini jana ukikutwa na matundu ya risasi.

Taarifa zinasema kuwa marehemu ambaye alikwenda mapumziko nyumbani kwao Muhange akitokea Kakonko, mwili wake uligundulika porini na ulikutwa bastola yenye risasi tano na pembeni kulikuwa na simu mbili za mkononi.
“Taarifa za daktari zinaonesha kuwa marehemu alinyongwa shingo na kupigwa risasi,” alisema mtoa habari wetu kutoka wilayani Kibondo.

Uchunguzi umebaini kuwa watu hao hawakuwa na dhamira ya kumuibia kwani hawakuchukua kitu chochote kwani hata simu zake mbili za mkononi zilikutwa zimetelekezwa kando ya mwili wake.

Hata hivyo taarifa zaidi zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo, zikiwemo sehemu nyeti.
“Hawa wauaji walikuwa na lengo la kutoa uhai maana hawakumuibia fedha wala simu kwa kuwa marehemu alikutwa na noti ya shilingi 10,000 mfukoni,” alisema.

Taarifa za kipolisi kutoka mkoani Kigoma zinasema kuwa kazi ya uchunguzi wa tukio hili imeanza wakati taratibu za mazishi zinafanyika.

No comments: