Sunday, January 27, 2013

Mtwara haitawaliki ni vurugu tupu, na milio ya risasi

Jengo la Mahakama likiteketea moto baada ya kuchomwa na watu wasiojulikana
 Kutoka Mtwara habari zinasema kuwa polisi jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wa Kata ya Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani, baada ya kuizingira nyumba ya Diwani Mohamedi Chehako kwa madai kuwa alikuwa amewahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Maria Nzuki hakupatikana kupitia taarifa ya simu yake ya mkononi.
Habari zilizolifikia  zilieleza kuwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliingilia kati vurugu hizo na kuanza kutembeza mkong’oto kwa wananchi kwa lengo la kuwatawanya.Taarifa zinasema kuwa askari hao waliingilia tukio hilo baada ya mwenzao aliyekuwa akipita eneo hilo kujeruhiwa na kutoa taarifa kwa wenzake waliofika na kutembeza mkong’oto kwa wananchi hao.

Baada ya askari hao kuondoka, wananchi hao walifunga kwa mawe makubwa njia zote kutoka eneo la mahakama, ambapo polisi waliegesha magari yao, hivyo kuwafanya polisi washindwe kutoka eneo hilo na wao kupata upenyo wa kuendeleza vurugu na uharibifu.

Habari ziliongeza kwamba wananchi hao walichoma jengo la choo cha mahakama na kuichoma moto nyumba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na kuvunja vioo vya nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Mohammed Sinani.

Wananchi hao walivamia nyumba ya diwani huyo baada ya kukuta ‘ungo’ unaodaiwa kutumiwa na watu wanaodaiwa kuwa wachawi kutoka sehemu moja kwenda nyingine pamoja na tunguri katika uwanja wa diwani huyo maeneo ya Makaburi Msafa.

Baada ya kushuhudia vitu hivyo, wananchi hao walijikusanya nyumbani kwa diwani huyo na kumshinikiza awatoe nje wachawi hao ili waweze kuwaadhibu, amri iliyopingwa na diwani huyo.

Kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo wananchi walivyozidi kuongezeka, ambapo baadaye kuliibuka kundi jingine la watu walioanza kuizingira nyumba ya diwani huyo, kumfanya diwani huyo kuomba msaada polisi.

Mashuhuda wa tukio walieleza kwamba polisi walipofika waliwasihi wananchi kutawanyika kwa kuwa ungo na tunguri hizo zilikuwa zimeteketezwa kwa moto na diwani huyo mbele ya wananchi hao.

“Wananchi waliendelea kupinga na kudai ndani ya nyumba kuna rubani na abiria wa ndege (ungo) wamehifadhiwa, kuona hivyo polisi wakawachagua wananchi watano na kuingia ndani ya nyumba kuwasaka watu hao, lakini hawakuona kitu, walitoka nje na kuwaeleza wenzao ambao hata hivyo walikataa kuamini maneno yao,” alisema Mussa Chehako na kuongeza:
“Walianza kurusha mawe katika nyumba ile na kuwafanya polisi kujibu mapigo kwa kurusha mabomu ya machozi .”

Alisema kuwa ni kawada yake kuamka alfajiri kwa ajili ya sala ya asubuhi, lakini asubuhi ya jana alishindwa kuamka mapema, hata hivyo hakuweza kuhisi jambo lolote.

Katika mapambano hayo ya wananchi na polisi, wananchi kwa kutumia mawe wamemjeruhi kwa jiwe kichwani Mwandishi wa Habari wa Channel Ten mkoani hapa, John Kasembe ambapo alitibiwa Zahanati ya Fajima na anaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Kasembe alipigwa mawe kichwani akiwa kazini kukusanya habari na wananchi waliokuwa

Ofisa wa Polisi ambaye jina lake hakutaka litajwe kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa gari moja ya polisi limevunjwa kioo cha mbele kwa mawe.

Hadi saa 10.00 jioni bado polisi walikuwa wanaendelea kupiga mabomu ya machozi hewani huku wananchi wakionekana kujipanga katika makundi hali iliyotishia usalama wa maeneo hayo.

Jijini Dar es Salaam, askari mgambo wawili wa Manispaa ya Ilala wamejeruhiwa vibaya jana, baada ya kutokea mapambano kati yao na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga eneo la Kariakoo.

Katika vurumai hizo, wanamgambo watano wametiwa mbaroni na polisi kwa madai kuwa ndiyo chanzo cha vurugu hizo.

Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Kipolisi Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi aliliambia gazeti hili jana kuwa, vurumai hizo zilitokea baada ya kutokea mzozo baina ya mgambo hao na polisi.

Alisema polisi walifika eneo hilo kuwakamata mgambo, ambao wanatuhumiwa kuwapiga Wamachinga katika Mtaa wa Agrey, juzi.

Minangi alisema kuwa juzi Wamachinga walipigwa na mgambo hao na kupoteza mali zao, hivyo wakaamua kwenda kushtaki polisi.
“Polisi walipopata malalamiko ya wamachinga hao walienda leo (jana), kuwasaka mgambo hao na walipokuwa wanataka kuwakamata, mgambo wenzao wakapinga wakisema; hapa hatoki mtu,” alisema Minangi.

Alifafanua kuwa katika kujibizana mgambo hao walikuja juu ambapo miongoni mwao walitaka kuwanyang’anya polisi silaha walizokuwa nazo.

Kamanda huyo alisema polisi walionekana kuzidiwa nguvu na mgambo hao, ndipo wamachinga wakaingilia kati na kuwapiga.

Alisema kuwa Wamachinga hao walionekana kuwa wengi na waliwaelemea mgambo hao kwa kuwashushia kipigo kama cha wezi.
Alieleza kuona hivyo, polisi waliokuwepo eneo hilo walijaribu kuwaokoa, lakini ikashindikana ambapo ilibidi wawapigie simu wenzao ili kutoa msaada.

Source: Mwananchi

No comments: