Thursday, January 10, 2013

Wanasheria Wamjia juu Kikwete kuhoji Mahakama kumvua Ubunge Dk Kafumu

English: Jakaya Kikwete at the World Economic ...
 Jakaya Kikwete .
KITENDO cha Rais Jakaya Kikwete kuhoji hukumu iliyomwengua Dk Dalaly Peter Kafumu kuwa Mbunge wa Igunga, kimewakera baadhi ya wanasheria nchini ambao wameeleza kuwa hatua hiyo ni kuingilia uhuru wa mhimili mwingine wa dola.

Akizindua Daraja la Mbutu mkoani Tabora, Januari 7, mwaka huu, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, alihoji uamuzi uliomwengua katika nafasi ya ubunge Dk Kafumu kwa kigezo cha kufanya kampeni kwa kutumia ujenzi wa daraja hilo.

Rais Kikwete alihoji mantiki ya uamuzi huo wakati ujenzi wa daraja hilo ni moja ya mambo yaliyopo kwenye Ilani ya CCM ya 2010 – 2015.

“Mwaka 2010 katika Uchaguzi Mkuu nilifika hapa kumnadi aliyekuwa mbunge wa jimbo hili, Rostam Aziz na ujenzi wa Daraja la Mbutu ni moja ya mambo yaliyopo kwenye ilani yetu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Katika uchaguzi mdogo baada ya kujiuzulu Rostam, CCM iliendelea kunadi ilani yake ya kujenga daraja hilo kwa kuwa lilikuwa halijakamilika baada ya mbunge wake kujiondoa.”

Akizungumzia kauli hiyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society (TLS), Francis Stola alisema hukumu hiyo ilikuwa sahihi kwani ni makosa kwa kiongozi wa Serikali kutumia jukwaa la kampeni za kisiasa kuzungumzia masuala yanayohusu utendaji wa Serikali akisema kufanya hivyo kunaweza kutoa ushawishi kwa wapigakura na kuvuruga mwenendo wa uchaguzi.“Kiongozi wa Serikali haruhusiwi kutoa kauli ambayo kwa namna moja au nyingine, inaweza kutibua mwenendo wa uchaguzi au kufanya wapigakura wasiwe na uamuzi huru,” alisema Stola na kusisitiza kuwa katika nchi inayosimamia misingi ya demokrasia na utawala wa kisheria, viongozi wa Serikali hawapaswi kutumia rasilimali za umma kwa ajili ya kupata mtaji wa kisiasa.”

“Ndiyo maana pia hairuhusiwi wakati wa kampeni kumwona kiongozi wa Serikali akitumia rasilimali za umma kama vile kutumia magari ya Serikali kuendesha kampeni za kisiasa,” alisema Stola.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema suala hilo linahitaji utafiti na siyo la kulizungumzia juujuu.

“Hilo ni suala la kiutafiti bwana. Fanya utafiti wako halafu uje tujadiliane.”
Wakili wa kujitegemea, Mpale Mpoki alisema Serikali haipaswi kutoa ahadi za kufanya jambo fulani wakati wa kampeni kwa kuwa hilo ni jukumu ambalo lilipaswa kufanywa bila kusubiri uchaguzi.

“Hata mgombea mwenyewe awe wa chama tawala au chama kisichokuwa madarakani, hapaswi kutoa ahadi kama zile za kujenga barabara, daraja au kufanya jambo lolote.”

“Kwa mtazamo wangu ni makosa mbunge akienda kwenye kampeni kujitangaza kwamba yeye mwenyewe akiwa mgombea atajenga daraja. Kujenga daraja au barabara si kazi ya mbunge, akifanya hivyo atakuwa akiwarubuni wananchi na inakuwa mbaya zaidi Serikali inapofanya hivyo.”

Wakili wa aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, Profesa Abdallah Safari alisema kwa kauli hiyo, Rais Kikwete amevunja Katiba. Alisema akiwa msimamizi mkuu wa katiba, hakupaswa kutoa maoni wala kuzungumzia hukumu ya Mahakama.

“Hata hivyo, kilichomwondoa Dk Kafumu siyo Daraja la Mbutu tu, hoja zilikuwa nane. Kwa nini Rais aione hiyo ndiyo ya maana kuliko hoja nyingine?”

Profesa Safari alihoji sababu ya Dk Magufuli kutofika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara tatu.

Hata hivyo, Wakili Twaha Taslima alisema kujinadi pekee kwa jambo au mambo ambayo mgombea na chama chake wanatarajiwa kuyafanya kama watachaguliwa, si tatizo.
“Hizo ni ahadi tu, watu wanategemea kukuchagua kwa ahadi kuhusu matatizo yao yanayowakabili,” alisema Wakili Taslima.

Alisema ikiwa ahadi iliyotolewa na mgombea iko kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chake na akiweza kuthibitisha hilo, haiwezi kuwa tatizo na kwamba sheria inaruhusu ahadi na kuelezea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama, isipokuwa tu kwa yale ambayo sheria hairuhusu.

“Mambo ambayo sheria hairuhusu ni kumshambulia mgombea mwingine kwa jinsi alivyo kama vile ulemavu, ubaguzi wa kijinsia, kama ilivyodaiwa kutokea katika kesi ya Jimbo la Arusha Mjini na ubaguzi mwingine wa aina yoyote,” alisema.

Wakili Majura Magafu alisema kampeni za uchaguzi zinatawaliwa na Sheria ya Uchaguzi ambayo Kifungu cha 108 ndicho kinachobainisha mambo ambayo hayapaswi kufanywa au kuzungumzwa na mgombea yeyote awe wa chama tawala au kinginecho.

Alisema hukumu iliyotolewa na mahakama kuhusu Dk Kafumu ilijichanganya kwa kuwa sheria inamkataza waziri mwenye dhamana husika kuahidi vitu ambavyo havipo kwenye ilani au mipango ya chama.
Kutokana na hali hiyo, alisema Waziri wa Ujenzi hakufanya kosa kuzungumzia juu ya Daraja la Mbutu kwa kuwa lilikuwapo kwenye Ilani ya CCM pamoja na ahadi za Rais.

Kilichomng’oa Kafumu

Mbali na Mahakama kueleza kuwa Dk Magufuli alitumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Igunga, Jaji Mary Shangali alitaja sababu nyingine kuwa ni ugawaji wa mahindi ya kuwawezesha wakazi wa Igunga kukabiliana na njaa wakati wa uchaguzi na kauli ya Imamu Swaleh Mohamed wa Msikiti wa Ijumaa Igunga, kuwatangazia waumini wa msikiti huo kuwa wasikichague Chadema kwa kuwa baadhi ya viongozi wake wamemdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

Hoja nyingine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kudai Chadema kilipeleka Igunga makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuvuruga uchaguzi.

Source: Mwananchi

No comments: