Thursday, February 14, 2013

Baada ya vurugu: Matangazo live bungeni kupigwa marufuku


Watangazaji wa TBC wakirusha matangazo ya bunge moja kwa moja kutoka Dodoma sasa uhondo huu unataka kutiwa kabali kutokana na vurugu zilizotokea hivi karibuni bungeni

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limesema linakamilisha taratibu za kusitisha kuonyesha matangazo yanayorushwa moja kwa moja na vituo vya runinga nchini kama njia ya kurudisha hadhi ya chombo hicho kwa jamii.

Uamuzi wa Bunge, umekuja siku chache baada ya kutokea vurugu zilizohusisha wabunge wa kambi ya upinzani, wakidai Spika Anne Makinda na naibu wake, Job Ndugai wamekuwa wakitoa upendeleo kwa wabunge wa chama tawala.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thamas Kashililah, alisema kuanzia vikao vijavyo vya Bunge, vitakuwa vikirushwa vile vilivyofanyiwa usanifu badala ya kuonyesha moja kwa moja ‘live’ kama ilivyozoeleka kwa wananachi.

Alisema hivi sasa ofisi yake, imeshawasilisha mapendekezo yake ambayo yapo katika hatua za mwisho, yakiwemo ya kurejea utaratibu wa zamani wa kutoonyesha vipindi vya moja kwa moja kutoka bungeni na badala yake Bunge liko mbioni kuanzisha chaneli yake ambayo itakuwa ikirusha matangazo yake.

“Leo kinachofanyika ndani ya Bunge ni kutokana na mifumo ya mawasiliano kukua na kutokana na hali hiyo, imekuwa ikitumiwa vibaya na baadhi ya wabunge ambapo badala ya kujenga hoja kwa maslahi ya wananchi, wamekuwa wakifanya vituko, hali inayoonekana wazi mhimili huu kupoteza heshima kwa jamii.

“Tumependekeza jambo hili na hivi sasa tutakuwa na utaratibu wetu wa zamani ambapo vipindi vyote, vitakavyorushwa ni vile ambavyo vimefanyiwa usanifu tu na sio vya kurushwa moja kwa moja kama ilivyozoeleka. Ninajua uamuzi huu kuna baadhi ya wabunge wataupinga, lakini huo ni ukweli wenyewe.

“Tupo katika mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuona namna bora ya kuhakikisha wanatupatia chaneli yetu ambayo tutakuwa tukiendesha sisi wenyewe. Lakini hata kama itakuwa ni TBC, basi tutawapa taratibu zetu za kurusha vipindi vyetu. Ni wazi kabisa kinachofanyika hakitofautiani na michezo ya kuigiza.

Spika Makinda
Akizungumzia hatua ya baadhi ya wananchi kumtumia ujumbe mfupi wa simu, Spika Makinda pamoja na naibu wake, alisema kwa kushirikiana na TCRA, wameweza kuwabaini watu hao, huku akiahidi majina yao yatakabidhikwa kwa Mamlaka husika kwa ajili ya hatua za kisheria.

“Suala la kuwa na namba za simu za viongozi si baya, ila tatizo ni namna ya matumizi, sisi Bunge tulitoa namba za simu za viongozi wote kwa lengo la kurahisisha mawasiliano na wananchi, lakini katika kipindi zimeanza kutumiwa vibaya.

“Wale aliomtumia ujumbe wa simu Spika na naibu wake, tumeweza kuwabaini na wakati wowote kutoka sasa tutayakabidhi majina yote kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua za kisheria. Uzuri hatua ya kusajili namba za simu imetusaidia sana na kila mmoja ataitwa na kujieleza kwa nini aliamua kuvunja sheria na kumtukana Spika.

Vurugu Bungeni
Alisema katika Mkutano wa Kumi wa Bunge, Watanzania wamekuwa wakitoa tafsiri mbalimbali, ikiwemo kutokea vurugu, hali ambayo haikuwa hivyo.

“Suala la kelele bungeni ni jadi ya wabunge wachache na hili halikuanza leo, hasa katika nchi za mabunge ya Jumuiya ya Madola kama hapa kwetu. Na kilichofanyika si kigeni kwetu, kwani wakati huo lilikuwepo kwa CUF ambao walikuwa wakisema ni hatari kuliko ilivyo hivi sasa kwa wanavyofanya CHADEMA.

“Ila ninapenda kueleza jamii ya Watanzania, kuwa katika mkutano uliomalizika hapakuwa na mgogoro mkubwa wa kanuni, ila kumekuwa na tafsiri tofauti ya kanuni. Kwani kwa kutumia hansard zetu za Bunge tumeweza kuwabaini kila mmoja hasa wale waliosimama na kuwasha vipaza sauti. Ni wazi Kanuni ya 60 ndio huongoza Bunge kwa utaratibu mzuri kabisa.

Tetesi
Itakumbukwa mwaka jana, aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, January Makamba, katika taarifa yake wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu mjini Dodoma, alipendekeza matangazo ya Bunge yaondolewe kwa sababu yanaonekana kuwanufaisha zaidi wapinzani.

Alidai wapinzani, wamekuwa wakitumia mwanya huo kushambulia Serikali na kujitangaza.

Lakini mapema mwaka huu, Spika Makinda akitoa maoni mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya, alisikika akisema umefika wakati sasa wa spika ajaye asitokane na chama chochote cha siasa.
Source: Mtanzania

No comments: