Monday, February 18, 2013

Kikwete achachamaa ataka uchunguzi mauaji ya Padri

Rais Jakaya Kikwete
Rais  wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi ambapo ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya kila liwezalo kuwapata walihusika wa tukio hilo.

Katika taarifa yake Rais Kikwete amesema analitaka jeshi hilo lifanye uchunguzi wa kina ili kujua kiini cha mauaji hayo.

“Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.” imesema taarifa hiyo.

Alisema pia ameagiza polisi washirikiane na vyombo vingine vya usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.

Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.”

Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili lililoko Mji Mkongwe Zanzibar, Evaristus Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana jana asubuhi wakati akielekea kanisani kuendesha ibada.


Tukio hilo limetokea majira ya saa moja asubuhi wakati padri huyo akijitayarisha kwenda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtoni nje kidogo na Mji wa Zanzibar.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kawaida Padri Mushi huwa anakwenda kusalisha katika Kanisa la Mtoni na kwamba jana, baada ya kufika kanisani hapo wakati akitaka kuegesha gari lake walifika watu kwenye gari lake na kumfyatulia risasi na kisha kukimbia kusikojulikana.

Makamu Askofu wa kanisa hilo Zanzibar, John Mfoi alisema kuwa watu waliompiga risasi Padri Mushi walikuwa wapo kwenye pikipiki aina ya Vespa na walikuwa wakimfuatilia kwa nyuma wakati akieleke kanisani.
“Baada ya kufika karibu na kanisa alipigwa risasi na gari kupoteza mwelekeo kisha kwenda kuonga nyumba,”alisema na kuongeza: “Uchunguzi wa hospitali umegundua alipigwa risasi tatu mbili zimetolewa kichwani na nyingine haijulikani iliko.”


Hilo ni tukio la pili kutokea kwa padri kupigwa risasi Zanzibar baada ya Desemba 26, mwaka jana Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki, Mjini Zanzibar kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.


Akizungumzia tukio la jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema pamoja na kuthibitisha, alisema ametuma timu ya wapelelezi kwenda Zanzibar kuchunguza kwa undani kuhusu tukio hilo.


“Watu wasiojulikana wamempiga risasi Padri Mushi, na baada ya tukio alipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja na kufariki dunia. Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo,” alisema IGP Mwema.

Alisema hadi sasa watu watatu wameshakamatwa kuhusiana na tukio hilo na msako mkali unaendelea na kuchunguza tukio zima.


IGP Mwema alisema ametuma timu Zanzibar itakayoongozwa na Manaibu Kamishna wa Polisi wawili ambao ni Samson Kasalla na Peter Kivuyo wakiwa pamoja na Kamanda wa Operesheni wa jeshi hilo, Simon Sirro.


“Tumekuwa tukifuatilia nyendo hizi na hivi sasa tutapambana na wahalifu ipasavyo, vurugu zozote zile lazima tupambane nazo ipasavyo,” alisema Mwema na kuongeza: “Kama kwenye tukio hili kutakuwa na masuala ya kigaidi nayo tutachunguza.”
Alisema watawatafuta kwa udi na uvumba wale wote wanaochochea au kufadhili yanayotokea kwa kuwa wanachokifanya ni uhalifu.

Matukio kama hayo ya kihalifu yamekuwa yakitokea mara kwa mara Zanzibar ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja watu watatu walipigwa risasi maeneo ya Bububu na Mbweni, lakini hii ni mara ya pili kwa padri kupigwa risasi katika historia ya Zanzibar.
Mwinyi akemea
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amewaonya viongozi wa dini kuhusiana na matukio ya vurugu yanayoendelea kujitokeza nchini akisema kuwa Tanzania ni sawa na gunia lililokusanya mchanyanyiko wa watu wenye kufuata mikondo ya dini inayotofautiana. Hivyo hakuna dini inayoweza kujigamba ni bora zaidi ya nyingine.

Aliwataka viongozi wa dini kuwakemea waumini wanaojihusisha na mienendo korofi kwa kuwa bila kufanya hivyo taifa linaweza kutumbukia kwenye mgogoro wa kidini na kusababisha upotevu wa hali ya amani na mshikamano.

Rais mstaafu Mwinyi ambaye alikuwa akizungumza kwenye sherehe za Maulidi iliyoadhimishwa jana na waumini wa Madhehebu ya Shia, alisema kuwa Tanzania iko kwenye wakati mgumu ikiandamwa na misukosuko ya aina mbalimbali ikiwemo ile yenye sura za kidini na kisiasa.

Alisema kuwa Tanzania iliyosifikia duniani kwa ustaarabu wake wa amani na mshikamano sasa inaanza kupoteza mwelekeo kwa raia wake kuingia kwenye maisha ya hofu na kushindwa kuaminiana.


“Ngoja niwapeni mfano mmoja hata kama mfano huu utakuwa mbaya kwenu, lakini nataka muelewe maana yangu… Tanzania ni sawa na gunia lililokusanya watu wa aina mbalimbali, wapo wale wenye dini, kuna wale hawana dini na wapo ambao wana dini inayotofautiana na dini nyingine...Hakuna upande unaoweza kujivuna kuwa ni bora kushinda mwenzake,” alisema na kuongeza;


“Ni wajibu wote tuliomo ndani ya gunia hili kushikamana na kuvumiliana kwani tukisema huyu ni bora zaidi ya mwingine, hatutafika mbali.”


Alisema kuwa Watanzania wanapawa kujenga tabia ya kuvumiliana na kutatua tofauti zao kwa njia ya majadiliano bila kujiingiza katika matukio yanayoweza kuharibu amani ya nchi.

“Waswahili walisema, maneno matamu humtoa nyoka pangoni. Hivyo nawatamanieni viongozi wa dini kazaneni kuwahimiza waumini wenu kutojihusisha na mienendo hatarishi kwa amani yetu,” alieleza Mwinyi, ambaye alioongoza Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.

No comments: