Sunday, February 10, 2013

Maajabu: Chanjo ya UKIMWI yagunduliwa Tanzania


JOPO la Madaktari wa Chuo wa Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), limekamilisha utafiti wa chanjo mpya ya virusi vya Ukimwi, ambao umethibitisha kuwa chanjo ya DNA -MVA ilikuwa salama na yenye uwezo wa kufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Utafiti huo ulifanyika nchini kati ya mwaka 2007-2010 na 2008-2012.


Utafiti wa awali uliofanyika kati ya mwaka 2007 hadi 2010, ambao ulijulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 polisi na magereza wa jijini Dar es Salaam, ambao walipewa chanjo hiyo na baadaye kuachwa wakiishi maisha yao ya kawaida kwa muda wa miaka mitano.


Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Profesa Muhammad Bakari, aliyeongoza jopo la madaktari waliofanya utafiti huo alisema kuwa umezaa matunda na kuthibitisha kwamba chanjo ya DNA –MVA waliyopewa askari hao, ilikuwa salama na yenye uwezo wa kufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).


“Chanjo hiyo inaweza kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU kwa asilimia 100 kwa washiriki waliopatiwa chanjo zote tano. Haya ni matokeo mazuri sana kupita hata matarajio watafiti, pia ni ya muhimu katika harakati za kutafuta chanjo dhidi ya VVU,” alisema.


Profesa Bakari, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo wa MUHAS, alisema kwamba hakuna mshiriki aliyekufa, wala kupata athari za moja kwa moja kwa na kupatiwa chanjo kutokana na tafiti hizo.


Alisema kuwa askari walioshiriki utafiti huo walifanya hivyo kwa hiari yao hadi kukamilisha utafiti huo.

Alibainisha kwamba jopo la madaktari bado liliendelea na utafiti zaidi, ulioanza mwaka 2008 hadi 2012, ili kupata chanjo sahihi ya VVU kwa aina ya pili ya chanjo ijulikanayo kama TAMOVAC-01(Tanzania and Mozambique HIV Vaccine Program), iliyohusisha pia nchi ya Msumbiji.

“Hatukuishi hapo, utafiti wa pili (TAMOVAC-01), ulifanyika kati ya mwaka 2008 na mwaka 2012. Utafiti huu ulijumuisha pia nchi ya Msumbiji.


Profesa Bakari alisema kuwa utafiti nchini Tanzania ulihusisha washiriki 120, kati yao 60 wakiwa ni kutoka jijini Dar es Salaam.


Alibainisha kwamba kwa mara nyingine washiriki hao walitoka katika Jeshi la Polisi, Magereza na raia wa kawaida, huku wengine 60 wakiwa raia wa kawaida kutoka jijini Mbeya.

Mtaalamu huyo alieleza kwamba utafiti huo pia ulionyesha kuwa mchanganyiko wa chanjo ya DNA-MVA ulikuwa salama.

Profesa Bakari alibainisha kuwa matokeo ya awali ya utafiti wao yanaonyesha kuwa chanjo ya DNA, inaweza kutolewa katika dozi ndogo na bila ya vinasaba vyote kuwa katika mchanganyiko mmoja, huku akiongeza kwamba mchanganuo zaidi wa takwimu kwenye utafiti huo bado unaendelea.


Hata hivyo aliweka wazi kuwa pamoja na kukamilika kwa utafiti huo, walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo uelewa mdogo wa jamii, uliojenga dhana potofu kwamba washiriki walipandikizwa VVU.

“Changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu tafiti hizi uliofanya kujengeka kwa dhana potofu kwamba washiriki wanapandikizwa virusi vya Ukimwi. Hii si kweli, bali washiriki walipatiwa chanjo ya majaribio dhidi ya VVU,” alisema.


Aliongeza: “Utafiti huo umeonyesha kuwa hakuna mshiriki aliyepata maambukizi ya VVU kutokana na kupatiwa chanjo hii.”


Kwa mujibu wa Profesa Bakari gharama kubwa imetumika katika kufanya tatifi hizo ikizihusisha Jumuia ya Ulaya (EU) na Serikali ya Sweden.

“Tafiti hizi zina gharama kubwa. Ufadhili wa utafiti wa HIVIS-03 ulitoka Jumuia ya Ulaya na Serikali ya Sweden,” Profesa Bakari aliweka wazi.


Alifafanua kuwa utafiti wa kwanza wa chanjo ya TAMOVAC-01 na wa pili wa TAMOVAC-II umefadhiliwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Tafiti za Kisayansi kati ya nchi za Ulaya na Nchi Zinazoendelea ‘European and Developing Countries Clinical Trials Partnership’(EDCTP ).


Alisema katika kufanikisha tafiti hizo jopo la madaktari bingwa walishirikiana pia na taasisi Swedish Institute for Infectious Disease Control, (SMI), Karolinska Institutet (KI) Sweden, University of Munich Ujerumani na Imperial College London UK.


Zimo pia Mbeya Medical Research Programme (MMRP) Tanzania, National Institute for Medical Research (NIMR) Tanzania, National Institute of Health (NIH) Msumbiji, Maputo Central Hospital Msumbiji, Jeshi la Polisi na Magereza Tanzania pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).


Profesa Bakari alisema kwamba licha ya kukamilika kwa tafiti hizo, kwa sasa wameanza utafiti mwingine ili kukamilisha chanjo kamili ya VVU.


Alisema utafiti huo unaoitwa TAMOVAC-II1 ulianza mwishoni mwa mwaka jana, utahusisha washiriki 80 kutoka Dar es Salaam, 80 kutoka Mbeya na 38 kutoka Maputo Msumbiji.


Aliwataja walioshiriki katika utafiti huo kuwa ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Kisali Pallangyo, Mratibu wa Maabara wa MUHAS, Profesa Eligius Lyamuya na Mtaalamu wa Kinga na
Magonjwa Yanayosababishwa na Virusi, Profesa Fred Mhalu.Alisema upatikanaji wa wafadhili utasaidia kupatikana kwa chanjo kamili hapo baadaye na kwamba watafiti hao wamekuwa na matumaini makubwa.

“Wanapoanza utafiti mpya wa hatua hii ya pili ya majaribio ya chanjo ya VVU, matumaini yanajengwa zaidi kwenye ugunduzi wao wa uwezo wa chanjo iliyotumika kutokomeza ugonjwa wa ndui, ambao ulitikisa dunia kwa zaidi ya karne mbili,” alidokeza.


Ugonjwa wa ndui uligundulika miaka ya 1700 na kuwachukua watalaamu hadi mwaka ya 1960 walipofanikiwa kupata chanjo yake.


Hata hivyo, chanjo hiyo ilitangazwa rasmi na kuanza kutumika kwenye miaka ya 1970.

Matumizi ya chanjo ya ndui yalisimamishwa katika miaka ya 1990, baada ya kuthibitika kwamba ugonjwa huo umetokomezwa kabisa duniani.


Utafiti wa chanjo ya ndui ndiyo ulioweka rekodi ya kuchukua miaka mingi zaidi katika historia ya tafiti za magonjwa ya binadamu hadi sasa, huku Ukimwi ukiwa ni ugonjwa uliofanyiwa tafiti kwa mapana zaidi duniani kuliko magonjwa mengine.


Hivi karibuni utafiti wa RV144 uliofanyika Thailand, Marekani na Ulaya, ulionyesha matumaini ya kupatikana kwa chanjo ya Ukimwi.


Utafiti huo ulionyesha uwezo wa chanjo kukinga kiasi cha asilimia 30 ya maambukizi mapya. Hata hivyo wataalamu wanaeleza kuwa bado huo siyo uwezo mkubwa unaohitajika kwa chanjo.Chanjo hiyo walipewa watu 16,000, ambao hawakuwa na maambukizi ya Ukimwi, wanaume na wanawake.


Katika utafiti huo, walibaini kwamba maambukizi ya Ukimwi yalikuwa ni asilimia 31 yakiwa chini kwa waliopewa chanjo kuliko ambao hawakupewa.

Source: Mwananchi