Wednesday, February 20, 2013

Zanzibar bado mambo si shwari kanisa lachomwa moto


Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema

Siku chache baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi Padri Evarist Mushi Mjini Zanzibar, Kanisa la The Pool of Siloam lililoko katika Shehia ya Kianga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, limechomwa moto na watu wasiojulikana na kuharibu madhabahu yake.

Kuchomwa moto kwa sehemu ya kanisa hilo, kumetonesha kidonda cha kifo cha Padri Mushi ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani, Jumapili asubuhi mjini Zanzibar. Padri huyo anazikwa leo.


Akizungumza katika kanisa hilo, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai upande wa Zanzibar ambaye pia ni Naibu Kamishna wa Polisi, Yusuf Ilembo alisema tukio hilo limetokea kati ya saa tisa usiku na saa 10 alfajiri ya kuamkia jana.


“Mlinzi aliona watu watatu wakiwa ndani ya eneo la kanisa na alipowakaribia wakaendelea kupanda ngazi kwenda juu. Baadaye walirudi na kuanza kumrushia mawe akakimbilia nje kupitia dirishani. Ghafla akaona moto unawaka, kumbe walikuwa wamechoma viti vya plastiki vilivyokuwa ndani,” alisema Naibu Kamishna Ilembo.


Mlinzi huyo, Mussa Jackson alisema: “Niliona watu watatu wakipita na baadaye wakawa wanarusha mawe, mwisho nikakimbia na kumwambia jirani na kumpigia simu mchungaji msaidizi. Wakati nakwenda kwa jirani nikaona moto mkali unawaka kanisani, sikujua wameuwashaje.”


Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo, Penuel Elisha alisema tukio hilo ni la pili kwa kanisa hilo kwani mwaka 2011 zaidi ya watu 80 wakiwa na mapanga, nyundo na magongo walilivamia na kulivunja kabisa.


Alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwahi kuwasaidia katika tukio la jana.
Licha ya kutotaka kuonyesha uhasama na msikiti uliopo eneo hilo, Penuel alisema siku moja kabla ya tukio hilo viongozi wa msikiti huo walihoji uhalali wa kujengwa kwa kanisa hilo.


“Siku moja kabla ya tukio la mwaka 2011, viongozi wa msikiti walihoji uhalali wa sisi kujenga kanisa hapa. Sisi tukawaonyesha vibali vyote. Lakini kesho yake kanisa likabomolewa. Hatuna mgogoro na msikiti, kwanza hayo matukio ni ya kawaida tu hapa Zanzibar,” alisema Penuel.


Alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa uhasama kati ya msikiti na kanisa hilo, Imamu wa msikiti huo, Hassan Migirimu alikanusha akisema kuwa mzozo huo ulikuwa kati ya kanisa na Sheha Assed Mvita ambaye amefariki dunia.


“Sisi hatuna mgogoro na hilo kanisa aliyekuwa akihoji uhalali wake ni marehemu Assed Mvita. Hatujawahi kugombana na kanisa hilo hata siku moja,” alisema Imamu Migirimu.


Padri Mushi kuzikwa leo
Padri Mushi anatarajiwa kuzikwa leo eneo la Kitope na ibada ya mazishi itaanza saa nne asubuhi katika Parokia ya Mtakatifu Joseph Minara Miwili.


“Baada ya kikao cha Baraza la Walei tulikubaliana kuwa ibada ya mazishi itafanyika hapa Parokia ya St. Joseph Minara Miwili na mwili wake utazikwa Kitope wanakozi kwa viongozi wa kanisa,” Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augustino Shao alisema jana.

Akizungumzia sababu ya Padri Mushi kuzikwa Zanzibar badala ya kusafirishwa kwenda kwao Moshi mkoani Kilimanjaro, Askofu Shao: “Padri Mushi ameishi Zanzibar tangu akiwa na miaka 18 hivyo ni mkazi wa Zanzibar... Hakuna sababu ya kusafirishwa. Mimi ndiye niliyekuwa mlezi wake hivyo hakuna sababu ya kumpeleka kuzika kwa askofu mwingine.”

Source: Mwananchi

No comments: