Wednesday, March 20, 2013

Safari hewa za nje za Kikwete , wanjanja watafuta fedha


SAKATA la ufisadi wa fedha za safari za Rais Jakaya Kikwete, lililokuwa linawakabili watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, limechukua sura mpya.

Hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kubaini kuwa Kitengo cha Itifaki cha wizara hiyo kinahusika na wizi huo.
Watumishi hao wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wamebainika kuhusika na ufisadi wa Sh bilioni 3.514, zilizochukuliwa Hazina bila kufuata utaratibu.

Ilielezwa kuwa fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya safari za viongozi, zilichukuliwa kinyemela na kitengo hicho ambapo baadaye walikamatwa huku Waziri, Naibu wake pamoja na makatibu wakuu wakiwa hawapo kazini na hawakuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo.

Hayo yalibainika jijini Dar es Salaam, baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kutakiwa kutoa ufafanuzi juu ya wizi huo wa fedha na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa.

Naibu Waziri Mahadhi, alisema kuwa kutokana na uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU, ilibainika kuwa maofisa zaidi ya watano walichukuliwa hatua mbalimbali, akiwemo Mkurugenzi wa Kitengo cha Itifaki, Anthony Itatiro, ambaye alisimamishwa kazi huku akisubiri hatua zaidi.

Mahadhi, alisema hatua hiyo ya Mkurugenzi huyo kusimamishwa imefanywa kwa mujibu wa taratibu, ikiwemo kusubiri uamuzi wa Rais, kutokana na cheo chake kuwa chini yake.

Kutokana na hali hiyo, Naibu huyo Waziri, alisema kuwa wizara yake baada ya kubaini kuwa kuna fedha zilizochotwa Hazina kwa ajili ya safari za viongozi bila kuwepo kwa safari hizo za viongozi, moja ya hatua ya haraka ambayo ilichukuliwa na wizara yake ni kuomba msaada wa haraka kwa TAKUKURU, ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo.

“Kutokana na uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU kuhusu fedha hizo, ilibaini kweli zilichotwa Hazina kwa uzembe ama nia ya kuiba na hivyo wizara iliweza kuwachukulia hatua za haraka za kiutawala watumishi wote walio chini yake na yule aliye chini ya mamlaka ya Rais hivi sasa anasubiri hatua zaidi kutoka mamlaka hiyo ya juu kwetu.

“Pamoja na hatua hiyo, watumishi watano na zaidi waliohusika katika tukio hilo, wapo waliohamishwa idara, walioshushwa vyeo na wengine walishushwa ngazi za mishahara yao ikiwa kama adhabu,” alisema.

Majibu hayo ya Naibu Waziri Mahadhi, yalimfanya Lowassa na wajumbe wengine wa kamati hiyo kuzidi kumbana kwa kutaka maelezo ya kina baada ya uchunguzi wa TAKUKURU na hatua ya kutofikishwa mahakamani kwa watumishi hao.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri huyo alisema kuwa kutokana na ushauri uliotolewa na TAKUKURU, ilikuwa vigumu kuwashitaki watumishi hao, kwani hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja, ila walikuwa na mpango wa kuiba fedha hizo, hali iliyowafanya wawachukulie hatua za kiutawala pekee.

Mbali na Mkurugenzi huyo wa Itifaki, Anthony Itatiro, watumishi wengine wanaodaiwa kuhusishwa na sakata hilo ni pamoja na ofisa katika Idara ya Itifaki, Shamim Khalfa pamoja na Kaimu Mhasibu Mkuu, Kasim Laizer.

Wengine ni Mhasibu Deltha Mafie na karani wa fedha (mtunza fedha) aliyetambulika kwa jina la Shabani Kesi.

Hatua hiyo ya sakata la ufisadi wa fedha za safari za viongozi ilimfanya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuunda tume ya uchunguzi wa sakata hilo, ambayo aliipa mwezi mmoja ili iwe imemkabidhi ripoti.

Hata hivyo, Lowassa, aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje nchini, kuhakikisha inakusanya taarifa za kila ubalozi wa Tanzania nje ya nchi, zinazohusu sera ya diplomasia ya uchumi na masuala mbalimbali ya utalii.

Aidha wajumbe wa kamati hiyo, waliibana Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuitaka kuunda kitengo rasmi cha diplomasia ya uchumi katika kila ubalozi wa Tanzania, sambamba na kuhakikisha wanaimarisha uhusiano baina ya wizara na wizara.

Akizungumza kuhusu sera hiyo ya diplomasia ya uchumi na namna itakavyoinufaisha Tanzania, Lowassa, alisema pamoja na kuwepo kwa Sera hiyo, bado ushiriki wa balozi za Tanzania katika masuala ya uchumi wa nchi hauridhishi.

Source:Mtanzania

No comments: