Tuesday, March 19, 2013

Lwakatare afikishwa mahakamani ashtakiwa kwa ugaidi



Wilfred Lwakatare
Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Rwezaura wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu waki kabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kutenda kosa la jinai la kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.

Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, Wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza kuwa washtakiwa hao walifanya kosa la kula njama na kutenda makosa ya jinai kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.



Rweyongeza alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana katika eneo la King’ong’o katika wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama kwa kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Msacky, kinyume na kifungu cha 227 cha sheria ya kanuni ya adhabu.

Wakili huyo wa Serikali katika shtaka la pili alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya kosa la jinai kinyume na kifungu cha sheria cha 24 (2) cha Sheria dhidi ya Ugaidi, sura ya 21 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Alidai kuwa washtakiwa hao, Desemba 28, 2012 walishirikiana kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Msacky kinyume na kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi.
Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi, kinyume na kifungu cha 5 (a) cha sheria namba 21 inayopinga ugaidi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky.
Kwa mujibu wa shtaka la nne, Lwakatare anadaiwa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.

Aliongeza kudai kuwa siku hiyo ya tukio, Lwakatare akiwa mwenye nyumba, akijua, aliruhusu mkutano kati yake na Ludovick ufanyike katika nyumba yake kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya kigaidi dhidi ya Msacky.

No comments: