Sunday, March 31, 2013

Waliokufa jengo lililoporomoka Dar wafikia 22



Idadi ya watu waliokufa kutokana na kufukiwa na kifusi cha jengo la ghorofa 16 lililoporomoka juzi asubuhi jijini Dar es Salaam, imefikia 22.
Habari zilizopatikana kutoka eneo la uokoaji na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zinaeleza kuwa miili iliyopatikana imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya Lucky Construction Limited liliporomoka saa 2.30 asubuhi wakati mafundi na vibarua wakiendelea na ujenzi huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya Kinondoni, Ibrahim Kisoka ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya ujenzi, na Mhandisi Mshauri kwa pamoja wamejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi na hadi saa 8:00 jana mchana walikuwa wakihojiwa.
Awali Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemtaka mmiliki wa Kampuni ya Lucky Construction Limited ambaye ni Diwani wa Kata ya Goba, Kisoka na wahusika wengine kujisamilisha kituo cha polisi, kabla hawajaamua kutumia nguvu kumtafuta.
Pinda atembelea eneo la tukio
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika eneo hilo saa 3:41 asubuhi, kujionea hali ilivyo, lakini hakutoa tamko lolote. “Sina la kusema,” alisema Waziri Mkuu alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa kauli ya serikali kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyefuatana na Pinda, alisikika akimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha mchora ramani wa jengo hilo naye anatiwa nguvuni kwa kuwa jengo hilo lilikuwa la ghorofa 10, lakini likajengwa hadi 16. Mtu mwingine ambaye anatafutwa na jeshi la polisi kukamatwa ni Mhandisi Mshauri.
Lukuvi alimwagiza Kova kuwa watu waliokuwa karibu na jengo jingine la ghorofa 15 lililojengwa na mkandarasi huyo, kuhama mara moja na ubomoaji ufanyike bila kuleta madhara.
Mwenyekiti wa CUF
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitumia fursa hiyo kuitaka Serikali kuwabana makandarasi wasio na sifa kwani wanahatarisha maisha ya watu.
“Huu ni uzembe, wahandisi wa jiji walikuwa wapi? Wasimamizi na washauri walikuwa wapi hadi jengo linafikia ghorofa 16?” Alihoji Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba aliitaka Bodi ya Makandarasi (CRB) kufuta leseni ya kampuni hiyo, kwani imeonyesha kuwa haiwezi kusimamia ujenzi na hivyo kusababisha vifo.

Huzuni, vilio na simanzi
Vilio na huzuni viliendelea kutanda jana katika eneo hilo ambapo waokoaji walikuwa wakijitahidi kufukua vifusi na kuzingirwa na watu waliokuwa wakisubiri ndugu zao waliofukiwa na kifusi kutolewa.
Watu wengi tangu asubuhi walikuwa wamesimama karibu na eneo hilo huku wengi nyuso zao zikiwa zimegubikwa na simanzi na wengine wakilia. Mama mmoja aliyekuwa akilia mapema asubuhi katika Mtaa wa Mshihiri, alisema mwanawe ni fundi na jana hakurudi, lakini pamoja na kilio, alisema bado haamini kama mwanawe amepoteza maisha.
Mwingine aliyekuwa ameshikiliwa na wenzake, alisikika akisema miongoni mwa waliopotea ni mume wake aliyemuaga asubuhi kuwa anakwenda kibaruani lakini hadi usiku wa manane hakurudi hivyo ilibidi afike eneo hilo.
Mama mwingine wa jamii ya Kihindu aliyekuwa akilia, alizirai kabla ya kuzinduka baada ya kupatiwa huduma ya kwanza. Mama huyo alisema mtoto wake ni miongoni mwa waliokwama kwenye kifusi hicho.
Barabara zafungwa
Mbali ya watu hao barabara zote zinazoingia katika eneo hilo zimefungwa.Barabara hizo ni Mshihiri na Morogoro, Hazrat Abbas, Mali -Asia, Mali-Zanaki, Mtaa wa Zanaki, India na Indira Ghandhi.
Wachina walishangaa ‘zege’
Wachina wa Kampuni za ujenzi za China zilizopo nchini, Beijing Construction Engineering Group, BCEG iliyojenga Uwanja wa Taifa, na ile ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC) inayojipanga kwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ni miongoni mwa waliofika kusaidia uokoaji.Zoezi la kutafuta miili iliyokwama katika vifusi inaendelea, zaidi ya maiti 22 zapatikana.

No comments: