Monday, April 1, 2013

Waliokufa jengo lililoporomoka sasa 32, JK atembelea majeruhiRais Jakaya Kikwete akimtembelea mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika hosptali ya Taifa ya Muhimbili
Idadi ya watu waliokufa kutoka na ajali ya jengo kuporomoka jijini Dar es Salaam mwishoni imezidi kuongezeka na sasa imefikia 32 baada ya kikosi cha uokoaji jana kupata miili ya watu saba zaidi na hivyo kufikia idadi hiyo tangu zoezi la uokoaji lianze.
 Mmoja kati ya miili hiyo baada ya kuuchunguza, ulikutwa na kitambulisho cha kupigia kura kinachomtambulisha kwa jina la Salumu Mwaliko kutoka Kijiji cha Kwadeboma, Handeni mkoani Tanga.

Wakati huo huo Rais Jakaya Kikwete jana aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo ambao wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwapa pole.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Mifupa (Moi), Dk Cuthbert Mcharo alisema walipokea majeruhi sita na hadi jana walikuwa wamebakia wanne.
NHC kugharimia majeruhi, mazishi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema amepokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kwamba kuna majengo matatu ya ghorofa ambayo yanatakiwa kubomolewa kutokana na kuchakaa. Mbali na hilo, Mkuu wa Mkoa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatakiwa kulipa gharama zote za watu walioathirika na ajali ya Ijumaa iliyopita.
Alisema NHC wanapaswa kuwahudumia majeruhi wote pamoja na kugharimia mazishi ya watu waliopoteza maisha.

Majeruhi aeleza alivyopona kifo

Fundi ujenzi, Yusuph Abdallah ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi), ameeleza jinsi alivyonusurika kifo baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Ijumaa iliyopita.
Yusuph aliliambia Mwananchi akiwa wodini kwamba kilichomponya ni neema za Mungu kwani kabla jengo hilo kuporomoka yeye alikuwa ghorofa ya 15 kwenye jengo hilo katika Mtaa wa Indira Gandhi akiendelea na ujenzi.
Alieleza kuwa hakuwa anafahamu kinachoendelea, bali aliona ghafla jengo linaaanza kuporomoka, na baada ya hapo hakufahamu zaidi kilichotokea hadi alipojikuta yuko hospitalini.
“Kweli jengo lilipoanza kuporomoka sikutambua nini kinachoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo hapa Muhimbili,” anasimulia Abdallah.
Alisema anahisi alipoanguka alifunikwa na kifusi kilichomponda na kuvunja miguu yote.
Fundi huyo ambaye amefungwa plasta gumu (P.O.P) miguu yote, alisema hakuweza kuona watu waliomwokoa.
Mwingine aokolewa na mkewe
Mkazi wa Ubungo, Ally Mlela ambaye ni fundi madirisha anasimulia jinsi mke wake alivyomwokoa katika ajali hiyo baada ya kumtaka asiende kufanya kazi siku hiyo.
Akisimulia jinsi ilivyokuwa Mlela anasema siku ya tukio aliwasiliana na rafiki yake ambaye amepoteza maisha katika ajali hiyo na kumtaka aende akaonane na mkandarasi wa jengo hilo, ili ampe kazi ya kuweka madirisha.
“Majira ya asubuhi kati ya saa mbili na saa tatu hivi nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu jina maarufu anajulikana kama Tafu, ambapo alinitaka niende nikaonane na mkandarasi wa jengo hilo ili anipe kazi ya kuweka madirisha,” anasema Mlela.
Anasema wakati akijiandaa kutoka mke wake alimwambia siku hiyo apumzike asiende kufanya kazi naye akakubali, lakini haikupita muda mrefu mke wake alimfuata na kumuuliza amesikia taarifa kwamba kuna jengo limedondoka?
“Niliamua kwenda katika eneo la tukio na ndipo alipogundua kwamba eneo hilo ndiyo alipotakiwa kwenda kufanya kazi. Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea nilijaribu tena kumpigia simu rafiki yangu.Nikiwa bado kwenye eneo la tukio ghafla nikaona mguu ukitolewa kwenye mchanga na nilitambua ulikuwa mguu wa rafiki yangu baada ya kuona kiatu chake.”

No comments: