Saturday, March 30, 2013

Kikwete aagiza mmliki na Mhandisi jengo lililoporomoka akamatwe mara mojaRais Jakaya Kikwete akipewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Said Meck Sadik na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova baada kufika katika jengo lililoporomoka 


Sehemu ya jengo lililoporomoka
Rais Jakaya Kikwete ameagiza mmiliki  na mhadisi aliyekuwa akijenga jengo  lililoporomoka jijini Dar es Salaam na kuua watu watano na wengine 40 kufukiwa na kifusi akamatwe mara moja 
Rais Jakaya Kikwete alifika katika eneo la tukio saa 6:45 mchana na alipata maelezo mafupi ya tukio hilo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliyetumia dakika tisa, alimwambia Mkuu wa Mkoa na Kamanda Kova: “…mmiliki na mhandisi lazima wakamatwe mara moja.”
Kikwete baadaye alitikisa kichwa kuonyesha masikitiko na kuondoka.
Naye Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na majeruhi na kuahidi kuwachukulia hatua kali waliosababisha tukio hilo.

Kamanda Kova alisema wanawashikilia watu watatu kwa mahojiano ambao ni Mhandisi Mkuu, Mkaguzi Majengo na Mhandisi Majengo wote wa Halmashauri ya Ilala kwa mahojiano zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amesema kuwa biola shaka kuporomoka kwa jingo hilo kumesababishwa na uzembe.
“Huu ni uzembe kabisa…, kuna watu wamepewa kazi za kusimamia ambao inaonyesha hawakufanya kazi zao ipasavyo. “Wote waliohusika, tutawatafuta popote walipo na watatueleza…,” alisema.
Mkuu wa mkoa pia aliagiza kusitishwa kuendelea kwa ujenzi wa jengo pacha kama hilo hadi uchunguzi wa kina utakapofanyika kuona kama limetimiza vigezo.


Hadi sasa bado watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo hilo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.
 Jengo lililoporomoka
Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege, kweli walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50 ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya ghorofa hilo kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.
Habari zilizopatikana baadaye jana jioni zilidai kuwa mmiliki wa jengo, Ally Raza pamoja na mhandisi wa Kampuni iliyokuwa ikijenga jengo hilo ya Lucky Construction Limited walidakwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakijiandaa kutimka.
Wananchi wajitokeza kuokoa
Mapema Wananchi waliojitokeza kwa kushirikiana na askari polisi na mgambo wa Jiji walioanza kuondoa kifusi cha mchanga kwa kutumia mikono kutokana na kutokuwapo kwa vifaa vya kuondolea kifusi hicho.
Ilipofika saa 4.30 ndipo trekta (kijiko) moja lilifika na kushirikiana na wananchi ingawa halikuweza kuhimili kazi hiyo nzito na kuhitajika trekta maalumu la kubeba na si kuzolea ili kunusuru uwezekano wa kuhatarisha uhai wa waliofukiwa na kifusi.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Ilala, Kheri Kessy alisema,mwaka 2007 walitoa kibali kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na ‘Ali Raza Investment Limited’ kujenga jengo la ghorofa 10.
“Kibali tulichotoa sisi ni cha kujenga ghorofa 10 na mkaguzi wetu alikuwa anafuatilia kila hatua hadi ilipofika ghorofa ya 10 akawa amemaliza kazi yake,” alisema Kessy.
Alipotakiwa kueleza kwanini hawakuchukua hatua baada ya kuendelea kujengwa hadi kufikia ghorofa zaidi ya 16 alisema, wao kwa hilo hawahusiki ila kuna taasisi zingine za Serikali zinazosimamia majengo zinatakiwa kuulizwa.
“Kama nilivyosema,sisi tulitoa kibali cha kujenga ghorofa 10 na mkaguzi wetu alikagua hadi ghorofa ya 10 hivyo kama waliendelea kujenga sisi hatujui kwani kuna CRB (Bodi ya Usajili wa Makandarasi) au ERB (Bodi ya Usajili ya Wahandisi) wao ndio wanahusika zaidi watawaelezeni,” alisema Kessy.
 NHC yatoa maelezo
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana lilitoa taarifa yake kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa mradi wa ujenzi wa ghorofa hilo ulikuwa ukifanyika kwa ubia kati yake na Kampuni ya Ujenzi ya Ladha ya jijini Dar es Salaam, ambapo NHC lilikuwa na ubia wa asilimia 25.
Ilieleza kuwa mbia huyo alipaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalam wa ujenzi na washauri  waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika, kwani NHC ilitoa ardhi tu kwa ajili ya ujenzi huo na ubia ungekamilika mara baada ya jengo hilo kumalizika kujengwa.
“Mbia akishapata wataalam hao yeye ndio  anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa NHC imesimamisha utoaji wa miradi mipya ya ubia ili kuweza kutathimini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa miradi ya ubia na hivyo kuwezesha kutengeneza sera mpya.

 Mtoto aliyenusurika anena
Mtoto mmoja aliyekuwa akicheza mpira na wenzake katika eneo hilo, Ally Karim alisema walikuwa tisa wakicheza mpira mara akaona jengo linadondoka na yeye akakimbia.
“Kati ya hao tisa ni mimi pekee ndiye nilikimbia lakini wengine walifukiwa chini na watatu wameokolewa lakini wengine wanne bado wako chini ya huo udongo…,” alisema Karim.
Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo, Chacha Boniface alisema jengo hilo lilikuwa na vibarua wengi juu wakiendelea na ujenzi.
“Vibarua walikuwa wengi, wengine walikuwa wakichanganya kokoto, wengine wakijenga matofali na wengine wakipiga plasta, bado mafundi wote wamefukiwa na kifusi,” alisema Boniface na kuongeza:
“Achilia mbali hao vibarua na mafundi, chini kulikuwa na magari yanapita, watoto wakicheza na mama ntilie (mama lishe) wakiuza uza chai hivyo nafikiri si chini ya watu 40 wamefukiwa”.
Naye Idd Baka alisema gari yake aina ya Noah ambayo aliiegesha katika eneo hilo na kushuka kwenda dukani kwa manunuzi, ndani ya gari hilo alikuwamo mkewe na watoto wawili, nao pia wamefunikwa na kifusi.
“Bado nawasiliana na mke wangu kwa njia ya simu, (ilikuwa saa 8 mchana) kwani mimi nilishuka kwenda dukani kurudi nikakuta kadhia hii, sijui itakuwaje” alisema Baka kwa huzuni.
Naye jirani wa jengo hilo, Ramesh Abdallah alisema alijua jengo hilo litabomoka kutokana na kujengwa chini ya viwango.
Alisema ndani ya miezi sita ilikuwa tayari ghorofa 12 zimekamilika kujengwa, hali ambayo aliitilia shaka uimara wake.
“Hata ukiangalia mchanga ni mwingi kuliko saruji, angalia hata nondo zake si za kujengea ghorofa 16, hii ndio Tanzania na wajanja ndio wanaofaidi huku watu wakipoteza maisha kizembe,” alisema Abdallah.
Wanasiasa
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi James Mbatia ambaye pia ni Mhandisi alitoa ushauri kubomoa kuta za msikiti na kibanda kilichokuwa katikati ili kurahisisha uokoaji jambo ambalo halikufanyika.
“Kama unavyoona nafasi ni ndogo, tunatakiwa kuheshimu mawazo ya kila mmoja ambaye anakuwa na nia nzuri sasa angalia matrekta (matatu) nafasi ndogo,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Ujuzi wetu katika masuala ya uokoaji bado ni mdogo, wamekuja Askari wa JKT, je, hawa askari kweli wanafundishwa kupambana na majanga?” Alihoji Mbatia.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alisema kilichotokea ni matokeo ya rushwa na uzembe ndivyo vilivysababisha jengo hilo kuporomoka.
“Kweli unataka kusema hili jengo lilikuwa halikaguliwi? Kilichokuwa kikifanyika ni watu kula fedha bila kutekeleza wajibu wao hivyo tutaendelea kuangamia kama watu hawatakuwa makini katika sekta zao,” alisema Mtatiro.
Red Cross walia kukosa vifaa
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Dar es Salaam, Hidan Ricco alisema kuwa kazi ya uokoaji ilikuwa ngumu kwani walikosa vifaa madhubuti kwa kazi hiyo.
Alisema pia kuwa vifaa vilikuwa vya ‘kuungaunga’ kutoka taasisi mbalimbali ambavyo hata hivyo kwa kiasi fulani vilisaidia.
Alipoulizwa kuhusu ajali hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema sio kila mtu anazungumza kuhusu tukio hilo na kusisitiza kuwa atafutwe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik.

Naye Msajili Msaidizi wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Flora Mwombeki ambaye alikuwa eneo la tukio jana alisema bodi hiyo inautambua mradi wa ujenzi wa jengo hilo lililokuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Ltd.
 “Mimi sio msemaji wa CRB ila mradi huu tunautambua, kuhusu nani alikuwa mkandarasi siwezi kukujibu kwa kuwa sioni kibao kinachoonyesha kuwa ni kampuni ya Lucky, nadhani baadaye ukiwatafuta wahusika wakuu watakupa ufafanuzi,” alisema Mwombeki.
 Matukio mengine
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu jengo kuanguka, kwani Februari jengo la ghorofa nne lilianguka maeneo ya Kijitonyama Mpakani jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 9.
Licha ya ujenzi wa jengo hilo kusimamishwa miaka 10 iliyopita, familia ya marehemu iliendelea kuishi katika jengo hilo.
 Juzi 21, 2008 jengo la ghorofa 10 lilikuwa likiendelea kujengwa na Kampuni ya NK Decorators katika Mtaa wa Mtendeni Kisutu jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua mtu mmoja.
 Mwaka 2006 pia liliwahi kuporomoka jengo na kuua mtu mmoja ambapo baada ya tukio hilo, tume ya kukagua majengo iliundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa na ripoti yake ilikabidhiwa serikalini lakini mpaka leo hii ripoti hiyo haijawahi kutolewa hadharani.

No comments: