Thursday, May 2, 2013

Kima chini kiwe 740,000/- yasema TUCTA


SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limependekeza kima cha chini cha mshahara kiwe sh 740,000 kutokana na gharama za maisha kuzidi kupanda.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Mbeya na Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicolaus Mgaya wakati akisoma hotuba ya wafanyakazi kwa Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi – Mei Mosi.

Alisema kuwa TUCTA iliiomba serikali ipandishe kima cha mshahara kufikia sh 315,000 kwa kima cha chini tangu mwaka 2010, lakini haikuwezekana.
Mgaya alisema kuwa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yatakuwa na tija pale tu maagizo na makubaliano yatakapokuwa yanatekelezwa.
Pia Mgaya aliishauri serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi kutoka asilimia 14 ya sasa hadi tatu.
Badala yake TUCTA, imeishauri serikali kutumia vyanzo vyake vingine kutafuta mapato kuliko kuendelea kuwabana wafanyakazi.
Mgaya alisema kuwa misamaha ya kodi inayotolewa kiholela na serikali imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingesaidia kuboresha mishahara na mazingira mazuri ya kazi kwa wafanyakazi.
Alisema kuwa takwimu zilizopo zinaonesha kuwa uchumi unakua kwa asilimia 0.3, lakini hautakuwa na maana yoyote kama misamaha ya kodi inatolewa bila kujali hali ya maisha ya wafanyakazi.
Mgaya alisema kuwa serikali inapoteza kiasi cha sh trilioni 1.3 katika misamaha hiyo, na hivyo kuwanufaisha zaidi wawekezaji ambao pia ni waajiri.
“Mheshimiwa rais, nachukua fursa hii kumpongeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoh kwa kuweza kufichua wizi mkubwa wa fedha za umma unaofanywa na watumishi wasiokuwa waaminifu na kuomba hatua kali zichukuliwe dhidi yao kwa kuwa wanasababisha uchumi wa nchi uzidi kushuka,” alisema.
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Mgaya alisema izingatie haki kwa tabaka la wafanyakazi na mishahara iwe agenda ya kitaifa.
Pia aligusia hatua ya serikali kukopa katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kutorudisha, akisema inazidi kuwaongezea majonzi wastaafu.
Akihutubia katika kilele hicho, Rais Kikwete aliahidi kuwa mishahara ya wafanyakazi itapanda katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao na kwamba Waziri wa Fedha atatoa mchanganuo huo.
Kuhusu kodi kupunguzwa kwenye mishahara ya wafanyakazi, Rais Kikwete alisema suala hilo limeshazungumzwa kwenye vikao vya pamoja na TUCTA na kwamba Waziri wa Fedha katika hotuba yake ya bajeti atalitolea ufafanuzi.
Licha ya rais kutoa matumaini hayo, baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine zilikofanyika sherehe hizo, walionesha kunung’unika.
Wafanyakazi hao wengi wao wakiwa walimu, walisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete haina matumaini makubwa kutokana na madeni makubwa wanayoidai serikali.
“Yaani hapa tumekaa tu hakuna jipya, tulitegemea kuambiwa madeni yetu yatalipwa kabla ya bajeti mpya, lakini mambo ni yale yale, hali ni ngumu. Huu uchumi unaokua mbona sisi hatuuoni?” alihoji mmoja wa walimu.
Mbali na mafanikio mengi ya serikali yake aliyoyaeleza, Rais Kikwete pia alisema kuwa kadiri uchumi utakavyozidi kukua, serikali nayo itakuwa na uwezo wa kuongeza zaidi ajira za watumishi wa umma.
“Tulifanya kosa mwanzo kutoa fedha bila kutoa elimu ya ujasiriamali, kwa hiyo tunakusudia kutoa fedha kwa ajili ya mafunzo kwenye vikundi vya vijana na wanawake ili waweze kupata mikopo na kuweza kusimamia vizuri miradi yao,” alisema Rais Kikwete.

Source: Tanzania Daima

No comments: