Friday, May 31, 2013

Matokeo mapya yatoka : waliopata sifuri bado juu sasa ni asilimia 56


Bofya hapa uangalie matokeo yote kama yalivyo

Waziri wa Elimu Dr Shukuru Kawambwa

Wanafunzi 30,063 waliopata daraja sifuri katika matokeo yaliyopita, wameula baada ya kupandishwa hadi daraja la nne kutokana na ukokotoaji upya wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) 
Hata hivyo marekebisho hayo bado hayabadili sana ufaulu kwani badio waliopata daraja sifuri ni zaidi ya asilimia 50 ambapo sasa badala ya asilimia 65 sasa ni asilimia 56

Bofya hapa uangalie matokeo kamili
Marekebisho hayo yalifanyika baada ya kufutwa kwa matokeo ya awali yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu.
Kufutwa kwa matokeo hayo, ilikuwa ni utekelezaji wa sehemu ya mapendekezo ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, baada ya wanafunzi 240,909 kupata daraja sifuri kwenye matokeo yaliyotangazwa mara ya kwanza.
Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema sasa watakaokuwa na sifuri ni 210,846 sawa na asilimia 56.92 wakati wavulana wakiwa ni 104,259 na wasichana 106,587.
Hiyo ina maana kuwa sasa ufaulu umepanda na kuwa asilimia 43.08 badala ya ule wa kwanza ambao ulikuwa asilimia 34.5.
Dk Kawambwa alisema kutokana na ukokotoaji mpya wa matokeo ya sasa, idadi ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo kwa daraja la kwanza mpaka la nne imeongezeka na kufikia wanafunzi 159,747 kutoka 126,847.
Wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 3,242 wavulana wakiwa ni 2,179 na wasichana 1,063 ikiwa ni asilimia 0.88 ya matokeo yote, daraja la pili ni 10,355 sawa na asilimia 2.8 wavulana wakiwa 7,267 na wasichana 3,088.
Waliopata daraja la tatu ni 21,752 sawa na asilimia 5.87 wavulana wakiwa 14,979 na wasichana 6,773, daraja la nne ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 .
Tofauti na matokeo yaliyofutwa, ambayo watahiniwa waliopata daraja la kwanza walikuwa ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1997.
Waliopata daraja la tatu walikuwa 15,426, wavulana 10,813 na wasichana 4,613, waliopata daraja la nne 103,327, wavulana 64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903, wavulana 120,664 na wasichana 120,239.
Dk Kawambwa alieleza watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 480,029 na waliofanya ni 458,139 sawa na asilimia 95.44.
Alisema kuwa watahiniwa wa shule waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 411,225 na waliofanya ni 397,138 sawa na asilimia 96.57 huku wa kujitegemea wakiwa ni 68,804 na waliofanya ni 61,001.
Agizo la serikali
Dk Kawambwa alisema kuwa matokeo hayo yamefanyiwa kazi kwa kutumia mfumo wa `Fixed Grade Ranges’(ukokotoaji matokeo usiobadilika) badala ya ule wa zamani wa `Flexible Grade Ranges’ (ukokotoaji matokeo unaoweza kubadilika).
Mei 3, mwaka huu, Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta matokeo hayo na kusema kuwa yatatayarishwa kwa mfumo wa zamani wa `Flexible Grade Ranges’.
Lukuvi alisema kuwa, mapendekezo hayo yalitolewa na Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza na matokeo hayo na mapendekezo hayo yaliridhiwa na Baraza la Mawaziri.
Dk Kawambwa jana alisema kuwa, mfumo wa Fixed Grade Ranges ndiyo uliotumika na kuwa kuanzia sasa mitihani yote itakuwa ikitumia mfumo huo.
Alisema kuwa pendekezo la Serikali lilishindikana kutumika kwani isingewezekana kuchanganya mifumo miwili kwa wakati mmoja.
“Ni kweli kuwa Serikali iliagiza matokeo haya yachakatwe kwa mfumo wa 2011 ambao ulikuwa ni `Flexible Grade Ranges’, kitaalamu siyo sahihi kutumia mifumo miwili kwa wakati mmoja, kwa kuwa haya matokeo ya 2012 yalitumia mfumo wa `Fixed Grade Ranges’, isingewezekana kuubadili.
“Kwa hiyo tulishauriana serikalini tukakubali kufanya `standardisation’ (ukokotoaji) kwa mfumo wa `Fixed Grade Ranges’ kwani kama tungetumia mfumo wa zamani wa `Flexible Grade Ranges’ lazima yangetokea matatizo,” alisema.
Shule bora na za mwisho
Katika shule kumi bora, Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Kifungilo iliyoko Tanga imetolewa katika kundi hilo kwenye matokeo mapya na nafasi yake kuchukuliwa na Shule ya Wasichana ya Feza ya Dar es Salaam.
Baada ya ukokotoaji mpya bado St.Francis Girls ya Mbeya imebeki kwenye nafasi ya kwanza ikifuatiwa Marian Boys ya Pwani, Feza Boys ya Dar es Salaam, Marian Girls ya Pwani, Canossa ya Dar es Salaam, Rosmini ya Tanga, Anwarite Girls ya Kilimanjaro, St. Mary’s Mazinde Juu ya Tanga na Jude Moshono ya Arusha.
Shule 10 za Mwisho
Shule za Ungulu Morogoro, Mkumba na Tongoni za Tanga na Ndame ya Unguja zimetoka katika kundi hilo la shule za mwisho
Shule za mwisho katika matokeo haya zimeongozwa na Mibuyuni ya Lindi, Namndimkongo ya Pwani, Chitekete ya Mtwara, Kikale ya Pwani, Zirai ya Tanga, Matanda ya Lindi, Kwamndolwa Tanga, Chuno ya Mtwara, Maendeleo ya Pwani na Maendeleo ya Dar es Salaam.

No comments: