Friday, May 10, 2013

Mlipuko Arusha: Saud Arabia yatoa tamko kuhusu raia wake kukamatwa




Serikali za Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE) zimezungumzia kukamatwa kwa raia wake, ambao wanahusishwa na tuhuma za kurushwa kwa bomu kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Arusha, Jumapili iliyopita.
Watu watatu walifariki dunia na wengine 60, akiwamo Balozi wa Vatican nchini na Mwakilishi wa Papa, Francisco Montecillo Padilla wakijeruhiwa baada ya bomu kurushwa wakati wa ufunguzi wa kanisa hilo lililoko Parokia ya Olasiti.
Watu tisa wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo la kigaidi, kati yao Watanzania ni watano na raia wageni wanne.
Viongozi wa Serikali walikaririwa wakisema wageni waliokamatwa raia watatu ni wa Saudi Arabia na mmoja wa UAE ambao walikamatwa wakati wakiondoka nchini kupitia Namanga.

Balozi wa Saudi Arabia
Balozi wa Saudi Arabia nchini, Hani Momina alikaririwa na mashirika ya habari ya kimataifa akikiri kukamatwa kwa raia wa nchi yake na kusisitiza kwamba hakukuwa na ushahidi wa kumhusisha na shambulizi hilo kwani alikuja Tanzania kutalii.
Momina alisema alikutana na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kinachochunguza suala hilo kwenye kituo cha polisi anaposhikiwa raia wake akitaka kujua kama mtu wao amewekwa vizuri.
“Tuna matumaini makubwa kuwa wataachiwa na tutaendelea kufuatilia suala lao hadi tuone mwisho wake,” alisema Balozi huyo na kusisitiza kwamba hawaondoki Arusha.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya UAE, kupitia mtandao wa Twitter ilieleza kuwa inafuatilia kwa karibu suala la raia wake watatu waliokamatwa. Ilisema walikuwa wanafanya kazi kwa karibu na ubalozi wa nchi yao huko Tanzania ili kufahamu hatima ya watu wao.
UAE imesema inapinga kwa nguvu zote vitendo vya ugaidi na iko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania juu ya raia wake kuhusishwa na tukio hilo.
Majeruhi saba waletwa Dar
Majeruhi saba wa mlipuko huo walisafirishwa kwa ndege kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya hali zao kuwa mbaya.
Majeruhi waliosafirishwa jana ni Jenipha Joachim aliyeumia kwenye mapafu na miguuni. Alimpoteza mtoto wake, Patricia Joachim juzi.
Wengine ni Fatuma Tarimo, ambaye chembechembe za vyuma zimeingia tumboni, Apolinary Malasha aliyejeruhiwa miguu na jicho kutokana na masalia ya vyuma vya mabomu, Albert Njau ambaye amedhurika mbavu na mgongo na Faustin Shirima ambaye amekutwa na vyuma tumboni.
Wengine ni Gabriel Godfrey (9) ambaye ana chembechembe za bomu tumboni na miguuni na Athanas Mrema(14) ambaye amevunjika mbavu na pia ana chembechembe za vyuma tumboni.
Kutokana na tukio hilo, wabunge walichangia posho yao kwa kikao cha jana ambayo ni Sh200,000 kwa kila mmoja.
Utata aliyefariki KCMC
Jina la mtoto Patricia Assey (9) ambaye ni miongoni mwa waliouawa katika mlipuko wa bomu hilo lilizua utata jana kiasi cha kufanya uongozi wa Hospitali ya KCMC na polisi kuzuia mwili wake kwa muda.
Source: Mwananchi

No comments: