Monday, June 3, 2013

Katiba Mpya yakamilika kuandikwa, rasimu kuzinduliwa leo


Mwelekeo wa Taifa la Tanzania utaanza kujulikana leo mchana Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapozindua rasimu ya Katiba Mpya kwenye tukio la kihistoria litakalofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona kama rasimu hiyo itakuja na majibu ya maswali magumu, makubwa ya muundo wa Muungano, madaraka ya Rais, uteuzi wa mawaziri kutokana na wabunge, muundo wa wakuu wa mikoa/wilaya na muundo wa mihimili mingine miwili ya dola; Mahakama na Bunge.
Uzinduzi wa rasimu hiyo unafanyika baada ya Tume hiyo kufanyia kazi ya uchambuzi wa maoni ya wananchi. Maoni hayo yalitolewa na wananchi wapatao 1,015,564 kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na waliohudhuria mikutano ya moja kwa moja, waliotuma ujumbe mfupi wa simu (sms), barua pepe na kutumia mitandao ya kijamii.
Idadi ya makundi yaliyotoa maoni ni 170 zikiwamo asasi 22 za dini, kiraia 72, taasisi za Serikali 71, vyama vya siasa 19, viongozi na watu mashuhuri 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu hiyo ndiyo itakayopelekwa kwenye Mabaraza ya Katiba na itajadiliwa miezi mitatu ili kuona kama mapendekezo ya Tume hiyo baada ya kuchambua maoni hayo ya wananchi yanafaa au yanahitaji marekebisho.
Huo ni mwendelezo wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ulioanza mwaka jana baada ya Rais Jakaya Kikwete kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanza kukusanya maoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid uzinduzi huo utaonyeshwa moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) kuanzia saa nane mchana.
Taarifa hiyo iliwaomba wananchi kufuatilia uzinduzi huo kwa umakini ili waweze kujua kinachoendelea. Kuzinduliwa kwa rasimu hiyo kutaanzisha upya mjadala wa Katiba ambayo inatungwa kwa mara ya sita.
Katiba iliwahi kutengenezwa mwaka 1961 wakati Tanganyika ilipopata Uhuru, mwaka 1962 baada ya nchi kuwa Jamhuri, mwaka 1964 ilipoundwa Katiba ya Muda baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na mwaka 1965 ilitungwa Katika Mpya iliyodumu hadi mwaka 1977 baada ya vyama vya Tanu na ASP kuungana na kuifanya nchi kuwa chini ya utawala wa chama kimoja cha siasa.
Kwa upande wa Zanzibar kumekuwapo Katiba Tatu. Kwanza ni ile ya Uhuru iliyotungwa mwaka 1963, Mwaka 1979 ikatungwa Katiba nyingine na ya mwisho ni ile ya mwaka 1984.
Muundo wa Muungano
Kwa muda mrefu, suala la muundo wa Serikali mbili katika Muungano limekuwa mwiba katika siasa za Tanzania Bara na Zanzibar.

No comments: