Wednesday, July 10, 2013

CHADEMA yaunda kikosi cha ulinzi kujilinda, Polisi yawaonya

Walinzi wa CHADEMA wakimlinda Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe

Hapa ni walinzi  wa Rais Jakaya Kikwete

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea Arusha katika mkutano wa CHADEMA mwezi uliopita,  sasa wameamua kuanzisha kikosi cha ulinzi kitakachoundwa na vijana.

Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alibainisha hapo jana kuwa kikosi hicho cha ulinzi kitakachaoundwa na vijana kitapewa mafunzo na watatumika kuwalinda viongozi wa CHADEMA katika shughuli za kichama na kitaifa.

Mbowe alisema Jeshi la Polisi limeshindwa  kuchukua hatua stahiki kuwalinda viongozi wa vyama vya siasa, hivyo Kamati Kuu ya CHADEMA imeamua kutoa mafunzo ya kujilinda.

Alibainisha kuwa sababu ya kuanzishwa kwa makambi ya ukakamavu ni kwa ajili ya kuwalinda viongozi wa CHADEMA kwakuwa polisi wameshindwa kufanya kazi hiyo au wanafuata maelekezo ya viongozi wa CCM.

Alisema vikundi vya ulinzi vya CCM kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na polisi wamekuwa wakiendesha zoezi la kuwadhuru wafuasi wa CHADEMA kwa kuwakata mapanga, kuwachoma visu au kuwapiga marungu pasipo kuchukuliwa kwa hatua yoyote.

“Tunaonewa sisi, tunashitaki sisi na tunakamatwa sisi, na sasa kama chama tunasema hii inatosha. Ni lazima tutafute njia mbadala ya kujilinda, tutakuwa ni wajinga kuendelea kupiga magoti na kulia,” alisema Mbowe.

Kiongozi huyo alisema CHADEMA kimewaagiza vijana wa chama hicho waliopo sehemu mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe mafunzo maalumu ya ukakamavu kwa ajili ya kuwalinda viongozi wao.

“Mafunzo haya yatatolewa katika kambi maalumu zitakazokuwepo katika mikoa yote nchini…, kitengo cha ulinzi ndicho kitakachoratibu jambo hili,” alisema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso akizungumzia mikakati hiyo ya Chedema, alisema hatua inachukuliwa na chama hicho ni uvunjifu wa sheria kwa kuwa jeshi hilo lipo kwa ajili ya watu wote, hivyo mtu akienda kinyume na kuvunja sheria lazima atachukuliwa hatua.

“Nasema sheria itachukua hatua, polisi ipo na kazi zote zinakwenda vizuri hilo ndiyo jukumu la msingi la jeshi, nina hakika jeshi ni imara, Watanzania wote wapo salama,” alisema.

Alisema jeshi lilianzisha ulinzi shirikishi kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anajilinda na kumlinda jirani yake, hivyo sheria za nchi zipo wazi na majeshi yote yanaanzishwa kwa mujibu wa sheria.

Kuanika ushahidi hadharani wa mlipuko Arusha

Wakati huo huo CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetishia kuuanika hadharani ushahidi unaothibitisha polisi kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani mwezi uliopita na kuua watu wanne mkoani Arusha, huku kikiamua kuanzisha kambi za mafunzo kwa vijana nchi nzima kwa ajili ya kuwalinda viongozi wao.

CHADEMA imesema itauanika hadharani ushahidi huo iwapo Rais Jakaya Kikwete atakataa kuunda tume ya kimahakama itakayokuwa na jukumu la kusikiliza shauri hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kikao cha dharura cha Kamati Kuu, kilichoketi kwa siku mbili jijini humo kimejadili masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwemo siasa, rasimu ya katiba mpya na uanzishaji wa kambi za mafunzo ya vijana.

Alisema CHADEMA hawapo tayari kuwasilisha ushahidi wao kwa polisi ambao ndio watuhumiwa wakuu, bali wanataka Rais Kikwete aunde tume huru ya kimahakama.
Alisema isipoundwa tume hiyo ya kimahakama, watauweka wazi ushahidi huo kwa wananchi wakati ukifika.

Mbowe alisema watausambaza ushahidi huo kwa vyama, mashirika ya kiraia ya haki za binadamu ndani na nje ya nchi pamoja na ofisi za kibalozi za mataifa rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwataka waishinikize serikali kuunda tume huru ya kimahakama kuchunguza tukio hilo na mengine yanayofanana na hayo juu ya mauaji ya kisiasa.

Aliongeza kuwa serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Sera (Uratibu na Bunge) William Lukuvi imetoa kauli isiyostahili ndani ya Bunge kuwa CHADEMA wamejilipua kwa ajili ya kutafuta umaarufu.
“Tunalaani kauli ya serikali kupitia kwa Lukuvi, ni ya kitoto, kijinga na ya kiuendawazimu. Sisi hatuwezi kutafuta umaarufu kupitia damu za Watanzania.
“Kama umaarufu unatufikia kwa kazi tuzifanyazo kwa ajili ya wananchi, serikali inatafuta pa kushikia baada ya polisi kuhusishwa,” alisema Mbowe.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona Lukuvi akiwakilisha serikali na kujinadi kuwa CHADEMA wanahusika na mlipuko pasipo kuuweka hadharani kwa lengo la kukomesha hatua hiyo.

Mlipuko wa Arusha

Mbowe alisema baada ya kutokea mlipuko wa bomu katika mkutano wa mwisho wa kampeni ya chama hicho mkoani Arusha na kuua watu wanne na wengine 70 kujeruhiwa, CHADEMA ilitoa tamko kuwa viongozi wake ndio walilengwa katika shambulio hilo.

Alibainisha kuwa viongozi wa CHADEMA akiwamo yeye na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ni miongoni mwa watu waliokuwapo siku ya kufunga kampeni hizo za udiwani.

Alisema katika tamko walilotoa walibainisha ushiriki wa moja kwa moja wa Jeshi la Polisi juu ya mlipuko huo, na kwamba Kamati Kuu imeridhia tamko hilo baada ya kuelezwa ushahidi uliopo.

Kutokana na ushahidi huo, Mbowe alisema chama chao kimefedheheshwa na kauli ya serikali bungeni iliyolenga kulisafisha Jeshi la Polisi kutohusika.

Alibainisha kuwa serikali inafanya jitihada za makusudi kulihusisha tukio hilo na CHADEMA wakati inajua polisi ndio waliotenda uovu huo.
“Tunashangazwa na kitendo cha serikali kupuuza maafa yaliyowafika wananchi wa Arusha. Nyote mnafahamu rais wetu ni mtu makini katika kuhudhuria misiba na majanga mbalimbali, lakini katika hili hata kauli ya kutoa pole haijatoka utadhani waliopata kadhia hiyo si Watanzania,” alisema Mbowe.

Alisema Bunge ambalo ni taasisi ya kuwawakilisha wananchi lilishindwa kuchukua nafasi yake ya kusimamisha kwa muda shughuli zake au kutuma wawakilishi katika tukio hilo na badala yake viongozi wa serikali wamekuwa wakitoa kauli zenye utata.

Alisema Kamati Kuu imelitaka Bunge, kuueleza umma kama tukio la kulipuliwa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA, ni tofauti na mengine kama yale ya mlipuko uliotokea kanisani Olasiti, mabomu Gongo la Mboto au kuzama kwa meli ya Mv Skargit.
Aliongeza pia kuwa Kamati Kuu, imelaani vitendo vya fujo, kushambuliwa, kukatwa mapanga kuchomwa visu na kulipuliwa kwa mabomu viongozi wa CHADEMA.
Alibainisha kuwa licha ya matukio hayo, Jeshi la Polisi limeshindwa kuchukua hatua stahiki kwa watu waliohusika.

Rasimu ya katiba
Mbowe alisema Kamati Kuu ya CHADEMA, imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kukusanya, kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa rasimu.

Alibainisha kuwa CHADEMA imetambua na kuainisha mapendekezo mengine ya msingi ambayo yanastahili kuboreshwa zaidi katika rasimu hiyo.

Alisema msimamo na maazimio ya Kamati Kuu, juu ya rasimu ya katiba mpya yameainishwa na kuchapishwa katika kitabu maalumu watakachokizindua katika mkutano wa hadhara watakaoufanya wakati wowote kuanzia sasa.

CC yasikitishwa na Mtwara
Alisema Kamati Kuu imesikitishwa na hali ya sasa kwa wananchi wa Mtwara wanaopata madhila makubwa kutokana na vipigo wanavyopata kutoka kwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi (JWTZ) huku serikali ikikaa kimya juu ya hali hiyo.

Aliongeza kuwa wananchi wa Mtwara kwa sasa wanateswa na kiu yao ya kutaka kujua watanufaika vipi na gesi inayotoka katika mkoa wao, hali iliyowaingiza katika kadhia ya kubakwa, kupigwa na hata kuifanya Mtwara ionekane kama mkoa unaotawaliwa na jeshi.

Alisema hali hiyo ni hatari kwa mustakabali wa taifa, hasa katika kuhifadhi demokrasia kwa kile alichoeleza kuwa nguvu ya jeshi inaweza kusambaa katika mikoa yote na kulifanya Jeshi la Polisi lisiwe na kazi ya kufanya au nchi kutokuwa na utawala wa kidemokrasia.

No comments: