Wednesday, July 17, 2013

Maskini Meya wa Arusha kutoka CCM sasa mguu ndani, mguu nje

Meya wa Arusha Gaudence Lyimo (kulia) na Rais Jakaya Kikwete wakati Rais alipozindua jiji la Arusha hivi karibuni nafasi ya meya huyu sasa ipo mashakani baada ya CHADEMA kushinda udiwani wa kata zote nne za Arusha katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni
Kitendo cha Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa juzi, kimetafsiriwa kwamba ni kumfanya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kukalia kuti kavu. Kwa ushindi wake huo, Chadema kimefikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha wakati CCM kimebakiwa kuwa na viti 12 wakati TLP ina viti sita.

Pia Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti zaidi kwani ina nafasi moja ya viti maalum iliyokuwa ikishikiliwa na Rehema Mohamed aliyetimuliwa mwaka 2011.
Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema, Isaya Doita alisema jana kwamba ushindi wa juzi ni chachu katika msimamo wa chama chao kutaka uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha urudiwe akiamini kuwa alichaguliwa kimizengwe.
Doita ambaye ni Diwani wa Ngarenaro, alisema wana imani muda si mrefu Jiji la Arusha sasa litapata Meya ambaye amechaguliwa kwa misingi ya sheria.
Chadema ilitetea viti vya Kata za Themi, Kimandolu, Kaloleni na Elerai ilivyovipoteza baada ya kuwafukuza waliokuwa madiwani wake kwa kosa la kukiuka maagizo ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu mwafaka wa umeya.
Ushindi huo unakihakikishia wingi wa wajumbe katika baraza hilo la madiwani hivyo kuwa na fursa kumwondoa madarakani Meya Lyimo. Doita aliahidi kuwa chama hicho kitakaa leo kutoa msimamo kuhusu suala hilo la umeya wa Arusha.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alisema Chadema kisahau suala la kuchagua meya mpya kwani uchaguzi wake ulishapita.
Chatanda, ambaye pia anaingia katika vikao vya Baraza la Madiwani la Arusha kutokana na kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, alisema Chadema kinapaswa kufanya kazi na meya wa sasa.
“Unajua vikao hivi vinaongozwa kwa kanuni, kwa hiyo wingi wao si hoja ya kumvua meya au kulazimisha kupitisha mambo yao,” alisema