Thursday, August 22, 2013

Kikwete ateua makatibu wakuu wapya, Dr Mtasiwa Naibu Katibu Mkuu


Dr. Deo Mtasiwa
Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu wakuu kumi na mmoja na naibu makatibu wakuu 14 wapya katika wizara mbalimbali.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuni Mchome ambaye sasa anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deodatus Mtasiwa ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Tamisemi.
Mtasiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni walisimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari, mwaka jana kupisha uchunguzi dhidi yao, kutokana na kukithiri kwa migomo ya madaktari nchini, pamoja na utendaji wao kulalamikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema: “Mtasiwa ameteuliwa kwa kuwa uchunguzi dhidi yake haujaonyesha kuwa ana kosa lolote, lakini wenzake (Nyoni) na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo bado wanachunguzwa.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo amehamishiwa Ikulu kusimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kuwa Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Makatibu wakuu walioachwa kwa maelezo kuwa watapangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda (aliyekuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Kijakazi Mtengwa (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Omary Chambo (Uchukuzi), huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa akistaafu wa hiari.
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete ameanzisha kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), kitakachokuwa kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk Mtasiwa.
Aidha, aliwataja makatibu wakuu waliohamishwa wizara kuwa ni Florens Turuka kutoka Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Joyce Mapunjo kutoka Viwanda na Biashara kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makatibu wakuu wapya
Alisema Jumanne Sagini ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dk Servacius Likwelile ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Dk Patrick Makungu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Alfayo Kidata ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Dk Shaaban Mwinjaka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi. Uledi Mussa ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko.
Charles Pallangyo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu sasa anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Sihaba Nkinga ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Sophia Kaduma ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Naibu makatibu wakuu wapya
Naibu makatibu wakuu wapya wizara zao katika mabano ni Angelina Madete (Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira), Regina Kikuli (Ofisi ya Waziri Mkuu), Zuberi Samataba (Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi anayeshughulika na Elimu), Edwin Kiliba (Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi), Dk Yamungu Kayandabila (Kilimo, Chakula na Ushirika), Profesa Adolf Mkenda (Fedha-Sera), Dorothy Mwanyika (Fedha-Fedha za Nje na Madeni), Rose Shelukindo (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk Selassie Mayunga (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Monica Mwamunyange (Uchukuzi).
Consolata Mgimba (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Profesa Elisante ole Laizer (Habari, Utamaduni na Michezo) na Armantius Msole (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Waliohamishwa
Naibu makatibu wakuu waliohamishwa ni John Mngodo (Uchukuzi kwenda Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Selestine Gesimba (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii).
Injinia Ngosi Mwihava (Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Nishati na Madini), Maria Bilia (Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda Viwanda na Biashara na Nuru Milao (Maliasili na Utalii kwenda Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).
Aidha, Dk Donaldo Mbando amethibitishwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu kusimamishwa kwa Dk Mtasiwa.

No comments: