Saturday, August 24, 2013

CCM yamtimua Mwakilishi Zanzibar aliyepinga serikali mbili

Mansour Yussuf Himid

Baada ya Kamati Maalumu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kudaiwa kumvua uanachama Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, mwenyewe aimeibuka jana na kusema anasubiri uamuzi ya vikao vya juu vya chama vilivyoanza jana mjini Dodoma.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo ambazo Mansour amekiri kuzisikia zinaeleza kuwa uamuzi huo umetokana na yeye kudaiwa kupingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ambayo inaunga mkono muundo wa serikali mbili.
Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, 2013 katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambapo wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama mwakilishi huyo.
Uamuzi wa kumvua uanachama Mansour uliwasilishwa katika kikao hicho chini ya Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Dk Shein ndiye aliyeongoza kikao hicho, huku wajumbe wakiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mohamed Hija, Mbaruk Rashid Omari na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, huku mapendekezo ya uamuzi huo yakipelekwa mjini Dodoma kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Mambo mengine ambayo anadaiwa kufanya Mansour ni kuasisi Kikundi cha Kiislamu cha Uamsho ambacho kinadaiwa kuchochea vurugu visiwani humo.
Akizungumza  Mansour alisema, “Mimi sina cha ziada ninachosubiri ni uamuzi wa chama. Baada ya uamuzi wa chama ndiyo nitakuwa na jambo la kuzungumza, tusubiri tu wala tusiwe na haraka.”
Wakati Mansour akieleza hayo mwasisi wa chama hicho, Hassan Nassor Moyo alipinga uamuzi huo, akisisitiza kuwa kama utatekelezwa ni wazi kuwa Mansour atakuwa amenyimwa haki yake ya kikatiba.
Moyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano visiwani humo amesema hata yeye yupo tayari kufukuzwa uanachama kama ikionekana ana msimamo kama wa mwenzake.
Akizungumza wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deutsche Welle ya Ujerumani jana, Moyo alisema, “Kama wameamua kumfukuza siyo sawasawa, wanasema ametofautiana na msimamo au sera ya CCM ya kuwa na muungano wa serikali mbili, hiyo ni sera ya CCM, lakini serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na rais wa Zanzibar imetunga sheria ya mchakato wa Katiba Mpya na imeeleza wananchi, vikundi na taasisi.”
“Mansour ni sehemu ya watu hao ana haki ya kutoa maoni yake. Kupanga mikakati ya kumwondoa ndani ya chama ni kumnyima haki yake ya uraia.”
Alipoulizwa swali na mwandishi wa redio hiyo kuwa Mansour siyo raia wa kawaida, kwani mbali na kuwa mwanachama wa CCM aliyeshika nafasi nyingi ndani ya chama hicho na serikali pia ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi hivyo maoni yake yanaweza kukiathiri chama alijibu, “Pamoja na kuwa ameshika nafasi za juu za CCM, lakini kubwa ni kwamba Mansour ni raia, raia ana haki yake ya kutoa maoni tena kisheria kabisa.”

No comments: