Tuesday, September 27, 2011

Dunia yamlilia Profesa Wangari Maathai


Baadhi ya watu wakitia sahihi kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha mwanaharakati maarufu wa mazingira Marehemu Wangari Maathai

 Watu mbali mbali duniani wanaendelea kutuma salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha aliyekuwa mwanaharakati maarufu wa mazingira duniani na Mtunukiwa wa tuzo ya Amani ya Nobel Prof Wangari Maathai ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia siku jumatatu.
Marehemu Wangari Maathai enzi za uhai wake
Profesa Wangari Maathai alipata tuzo la amani ya Nobel mwaka 2004, kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Mbali ya kuwa Mwanaharakati wa Maswala ya Mazingira na haki za binadamu , Wangari Maathai pia alikuwa mwanasiasa shupavu. Amewahi kuhudumu kama Mbunge na Naibu waziri wa Mazingira nchini Kenya.
Prof Maathai pia katika uhai wake alipata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kutambua mchango wake.
Alipendwa na watu duniani hapa yupo na Rais wa sasa wa Marekani Barak Obama
Prof. Wangari Muta Maathai alianzisha vuguvugu la Green Belt mnamo mwaka 1977, ambapo alifanya kazi na wanawake kote nchini kuboresha maslahi yao na kuhifadhi mazingira.
Alikuwa mtetezi mashuhuri wa matumizi bora ya mali asili . Shughuli zake zilitambuliwa mara kwa mara kote duniani.
Marehemu ameacha watoto watatu, wawili wakiume na mmoja wa kike.


Mchango wake katika harakati za mazingira utakumbukwa daima hapa akipokea tuzo ya Nobel