Saturday, November 10, 2012

Kashfa ya Akaunti ya Vigogo Uswis Moto: Mwanasheria Mkuu akwama kuzima

Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Jaji Frederick Warema

NGUVU za Serikali za kutaka kuifuta hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto ya kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya nchi, jana zilishindwa baada ya wabunge kadhaa kumgomea Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kufanya hivyo.

Dalili za Serikali kutaka kuzima hoja hiyo zilianza baada ya Jaji Werema kusimama na kutoa mapendekezo ya kufuta vipengele muhimu.
Hatua hiyo ilizusha mvutano mkali, huku baadhi ya wabunge wakisema Serikali inataka kuifuta hoja hiyo muhimu kwa mustakabali wa taifa.


Mapendekezo ya Werema

Katika mapendekezo yake, Jaji Werema alipendekeza kufanyika kwa marekebisho kwenye kipengele katika hoja hiyo ya Zitto ambacho kiliitaka Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia Kitengo cha Assets Recovery Unit irejeshe nchini mabilioni ya fedha yanayomilikiwa na Watanzania katika benki za Uswisi na maeneo mengine yote ambayo hufichwa fedha ili kukwepa kodi.

Jaji Werema alitaka pendekezo hilo liondolewe kwa maelezo kuwa mamlaka za uchunguzi ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Usalama wa Taifa zinalifanyia kazi suala hilo.

Eneo jingine katika hoja ya Zitto ambalo Jaji Werema alipendekeza lifanyiwe marekebisho ni kuwapiga marufuku viongozi wa Serikali na watoto wao pamoja na Watanzania wengine kufungua akaunti nje akisema suala hilo litashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya fedha za kigeni.

Pia alitaka pendekezo lililomo katika hoja ya Zitto cha kutaja akaunti za watu wenye fedha benki za nje na kuzichapisha katika vyombo vya habari lifanyiwe marekebisho kwa kuondolewa.
Alisema suala hilo ni gumu na linakwenda kinyume na sheria za benki zinazotaka kutunza siri za wateja wao.
Kuhusu pendekezo la kuitaka Serikali katika Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/13 kuanzisha kodi maalumu ‘Financial Transaction Tax’ ya angalau asilimia 0.5 ya thamani ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na rekodi za uhakika fedha za ndani na zinazotoka nje ya nchi, Werema alitaka lifutwe akisema hiyo inahitaji utafiti wa kutosha.

Alisema ofisi yake imechukua siku nyingi kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ikiwemo kwenda Uswisi na kwingineko na kwamba itashirikiana na vyombo binafsi vya uchunguzi kufanya kazi hiyo.
Pendekezo jingine lililopingwa na Jaji Werema lilikuwa ni kuitaka Serikali kuwabana Watanzania wenye fedha nje ya nchi waeleze walikozipata akisema kazi hiyo inaweza kufanywa na Takukuru.

Wabunge wamshukia
Baada ya kutoa mapendekezo hayo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema anamshangaa Mwanasheria Mkuu kwa kufanya marekebisho ambayo yanaizima hoja ya Zitto.
Huku akinukuu vifungu vya Kanuni za Bunge, alisema Mwanasheria Mkuu anataka kuua hoja hiyo na kwamba mapendekezo yake yanakwenda kinyume na kanuni ambazo zinataka kila badiliko katika hoja liwiane na jambo linalojadiliwa.

“Hoja ya mabadiliko ya Mwanasheria Mkuu kuondoa mapendekezo hayo, kwa maoni yangu yanakinzana na Kifungu 53 (3) (4) cha Kanuni za Bunge, kinachopendekeza kuwapo kwa mabadiliko na siyo kufuta hoja.
Alisema hatua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kupendekeza mabadiliko hayo ni kufuta hoja jambo ambalo alisema ni kinyume cha kanuni. Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mtu ambaye anaweza kuiondoa hoja ni mtoa hoja na si mtu mwingine yeyote.

Alimtaka Spika kutumia busara yake kumzuia Mwanasheria Mkuu kufuta hoja hiyo muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Baada ya maelezo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na kuunga mkono mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu, huku akielekeza ‘makombora’ kwa Lissu kuwa anachokisema kinapingana na mtoa hoja Zitto, ambaye anakubaliana na Mwanasheria Mkuu.
Hata hivyo, Zitto alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa hakubaliani na mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu yanazima hoja yake.

Baadaye Lukuvi alisema anaunga mkono pendekezo moja katika hoja ya Zitto la Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya uchunguzi katika Bunge la 11 na kwamba ili kasi hiyo iende vizuri yashirikishwe pia kampuni binafsi ya uchunguzi.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alipinga pendekezo la kuiondoa hoja hiyo na kuunga mkono azimio kwamba Bunge liiagize Serikali kufanya uchunguzi huo na ripoti yake iwasilishwe katika Bunge la 11 na ikishindwa, Bunge liunde kamati ndogo ya kufanya kazi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia, aliuanga mkono mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisema vyombo vya uchunguzi viachiwe kuchunguza mabilioni ya fedha yaliyopo nje ya nchi.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alipinga akisema mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yalikuwa na lengo la kuua hoja hiyo akisema wabunge watafanya dhambi kubwa kuiondoa hoja hiyo ya msingi.
Sendeka alitaka hoja hiyo iboreshwe kwa kumtaka Zitto awataje hadharani watu ambao wameficha fedha nje ya nchi ili Watanzania wawafahamu... “Ukiwataja hawa hoja yako itakuwa na mashiko, tusaidiane na wala siyo fedheha kuwataja.”
Alitaka kamati iundwe kuchunguza jambo hilo ili ukweli ujulikane.

Baada ya kubanwa na wabunge, ndipo Jaji Werema alisimama na kulegeza msimamo wake kwa kurejesha pendekezo la Serikali kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi vya nje pamoja na wachunguzi binafsi kufanya kazi hiyo.
Alikubali pia pendekezo la kuitaka Serikali kuja na mkakati wa kueleza nini imekifanya katika Bunge la 11.
Aliwataka wabunge wote wenye majina ya watu walioficha fedha nje ya nchi kuyapeleka Takukuru au wamkabidhi yeye.

Baada ya hapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisimama na kusema hoja ya Zitto haikuwa mbaya na kusema Mwanasheria Mkuu pia alikuwa na nia njema.
Alisema Serikali haiwezi kumficha mhalifu akisema kama mtu ameiba atachukuliwa hatua bila ya kumwonea haya. Aliungana na Mwanasheria Mkuu kutaka Serikali iachiwe jambo hilo ilifanyie kazi.

Akihitimisha mjadala huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema hoja ya Zitto haijatupwa bali, inaingia kwenye utaratibu wa Serikali wa kuyatekeleza maazimio hayo.
Alisema Serikali itapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa hoja ya Zitto katika Bunge la 11 la Aprili) mwakani na kama ikishindwa, Bunge litaunda kamati kufanyia uchunguzi maazimio hayo.

Msimamo wa Zitto

Akizungumza baada ya uamuzi huo wa Bunge, Zitto alisema ameridhishwa na hatua hiyo akiamini kwamba itafanyiwa kazi.
Alisema amefurahi pia kwa kuwa hiyo ni mara yake ya kwanza kwa hoja yake kufanyiwa kazi na Bunge.

Source: Gazeti la Mwananchi

No comments: