Wednesday, December 5, 2012

Rufaa ya Lema moto! Mawakili Wapambana kwa vifungu

Godbless Lema akiwa na Mawakili wake kulia ni Wakili Tundu Lissu
 Rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), jana iliunguruma katika Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam, huku Wakili anayemtetea Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Vitalis Timon, akidai kwamba, Lema hakustahili kuvuliwa ubunge kwa kuwa alishinda kihalali.
Pamoja na hayo, Timon alidai mahakamani hapo, kwamba wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopinga ubunge wa Lema hawana haki ya kufanya hivyo na kwamba matusi hayawezi kumvua ubunge.

Kwa mujibu wa Timon, matusi hayawezi kumvua ubunge Lema, kwani wabunge wenyewe walitunga sheria namba nane ya mwaka 1995 ambayo inaruhusu matusi baada ya kuona awali walikuwa wakibanwa na mahakama.Wakili Timon alidai hayo jana, katika Mahakama ya Rufaa, mbele ya jopo la majaji watatu, Nathalia Kimaro, Salum Massati na Benard Luanda, wanaosikiliza rufaa hiyo iliyokatwa na Lema, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha wa kumvua ubunge.

Lema alivuliwa ubunge Aprili 5 mwaka 2012, kutokana na kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.

“Mpiga kura hawezi kupinga matokeo ya uchaguzi wakati yanayotokea katika kampeni hayamhusu, mpiga kura si sehemu ya Kamati ya Maadili na hana haki katika kampeni.

“Ushahidi uliotolewa ni matusi dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM ambaye ni Batilda Buriani.

“Ubaguzi wa kidini, kijinsia na makazi, mambo hayo yana athari gani kwa wanachama wa CCM waliofungua kesi ya uchaguzi namba 13/2010 Arusha?

“Hoja ya matusi mtu pekee aliyetakiwa kuipeleka mahakamani ni aliyetukanwa na si mwingine, Batilda mwenyewe yupo, haiwezekani mtu mwingine achukue matusi yake kisha akalalamike mahakamani kwa niaba yake.

“Pia, katika ushahidi inasemekana walalamikaji walimshauri Batilda kwa muda mrefu afike mahakamani ili kuthibitisha matusi yanayodaiwa kutolewa na Lema, lakini alikataa na ndipo walalamikaji wakaamua kwenda wao mahakamani.

“Julai 31, 1995, Bunge lilipitisha sheria namba 8 wakisema kwamba matusi si sababu ya kutengua matokeo, wenyewe wabunge waliruhusu watukanane katika sheria waliyotunga, wao wanapenda kutukanana.

“Wabunge walijipendelea wakati wakitunga sheria hiyo baada ya kuona mahakama inawabana katika eneo hilo, waacheni watukanane, waliyataka wenyewe.

“Wanaohusika wakati wa kampeni ni wagombea, vyama vya siasa, mawakala wa wagombea na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na pia wapiga kura wanahusika katika hatua za usajili wa wapiga kura na wakati wa kupiga kura.

“Waheshimiwa majaji, waliokuwa na masilahi binafsi katika kesi hii ni waliopoteza jimbo, kwani baada ya uchaguzi, CCM walikaa kikao na kuazimia kulirudisha jimbo kwa kufungua kesi, hawa walikuwa na nia mbaya walipofungua shauri hili.

“Sioni kwa nini Jaji wa Arusha aseme Lema alikuwa na maslahi binafsi katika ushahidi wake kwa kuleta wanachama wa CHADEMA kutoa ushahidi, angewaleta watu gani zaidi ya hao waliokuwapo wakati wa kampeni?

“CCM walileta mashahidi wa CCM, lakini hawakuambiwa kwamba walikuwa na maslahi binafsi, naunga mkono rufaa na naomba uamuzi wa kumvua Lema ubunge utenguliwe,” alisema.

Wakili wa Lema, Method Kimomogolo akizungumzia hoja 18 za kukata rufaa, alidai Jaji wa Mahakama ya Arusha alikosea kisheria kuvutiwa na njia wanazotumia kuishi mashahidi wa 11 na 14 badala ya kuzingatia uzito wa ushahidi waliotoa.

“Yule Jaji alivutiwa na shahidi wa 11 ambaye ni Amina Ally, anayeishi kwa kuuza mitumba na shahidi wa 14 ambaye alitumikia jeshi nje ya nchi na akastaafu kwa kuogopa kupelekwa tena nje ya nchi.

“Jaji alikosea kuegemea katika ushahidi usioaminika na ushahidi wa mdomo bila kutafuta ushahidi mwingine wa kuunga mkono hivyo kuifanya hukumu kutokidhi vigezo vya kuitwa hukumu,” alidai Kimomogolo.

Alidai jaji hakutumia mifano ya kesi mbalimbali zilizoamuliwa na Mahakama ya Rufaa, japo alipelekewa ili azirejee na mawakili wa pande zote mbili na pia hakuchanganua wala kupima ushahidi pamoja na kuwasilishiwa viini vikuu vilivyokuwa vinabishaniwa.

“Mrufani hakuwahi kukamatwa na polisi wakati wa kampeni kwa kutukana na jaji hakusema makosa gani ya jinai yalitendwa na mrufani katika kampeni zake,” alidai Wakili Kimomogolo.

Alidai uamuzi uliomvua ubunge Lema ukikubaliwa na kuruhusu kila mtu apinge matokeo ya uchaguzi kwa kufungua kesi hali itakuwa mbaya, katika hili mtu afike mahakamani kwa malalamiko yanayomhusu.

“Jukumu la kutetea maslahi ya taifa ni la Mwanasheria Mkuu wa Serikali wala si wanachama wa CCM waliopinga ubunge, kama wanaona AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) hafanyi kazi vizuri, wananchi wamwajibishe,” alidai.

Katika kujenga hoja ya maelezo yake, Wakili Kimomogolo alirejea kesi mbalimbali zinazofanana na kesi ya Lema na kuzitaja kesi ya Jaji Joseph Warioba dhidi ya Steven Wasira, Basil Mramba dhidi ya Leons Ngalai, William Bakari dhidi ya Mgonja na kesi ya Walid Kaburu iliyoamuliwa miaka 16 iliyopita ambapo watu waliwasilisha hadi mikanda ya sauti mahakamani.

“Kwa nini katika kesi ya Lema wajibu rufani hawakuwasilisha hata ushahidi wa ‘tape’ kuonyesha matusi aliyotukana,” alihoji wakili huyo.

Wakili wa wajibu rufani, Alute Mughwai alidai mashahidi wao walieleza kila kitu mahakamani na jaji alikuwa anajua nani mwenye jukumu la kuthibitisha kesi.

Alidai ushahidi uliotolewa haukupaswa kuungwa mkono na ushahidi wowote, siasa za uchaguzi zinatakiwa kuwa safi, kwani hata katika kanuni za uchaguzi wanaonywa kuhusu matusi, kejeli na kudhalilishana.

“Siasa za matusi ni siasa za maji taka, zilikatazwa, kanuni zilizokataza zilisainiwa na vyama vyote, watu wanachaguliwa kwa hoja si kuungurumisha matusi na kuwadhalilisha wagombea wengine,” alidai.

Kutokana na hali hiyo, alidai hukumu iliyomvua Lema ubunge ilikidhi viwango vyote na akaomba rufaa itupiliwe mbali kwa kuwa sababu zilizotolewa na mrufani hazitoshelezi kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

“Waheshimiwa tunaomba uamuzi wa Mahakama ya Arusha ubaki kama ulivyokuwa na warufani waamuriwe kulipa gharama za kesi,” alidai Wakili Mugwai.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi itakapopangwa siku ya kutoa hukumu.

Source: Mtanzania

No comments: