Tuesday, January 29, 2013

Juhudi za kumtoa Lulu kwa dhamana zakwama jana, Je leo atatoka?




MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali kumpa dhamana msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia.Msanii huyo alipewa dhamana hiyo jana kwa masharti manne ya msingi, likiwamo la kusaini bondi ya jumla ya Sh40 milioni.

Hata hivyo, licha ya Mahakama hiyo kumpatia dhamana, juhudi za mawakili wake, kuhakikisha anarejea uraiani jana hiyo ziligonga mwamba baada ya Msajili wa Mahakama aliyepaswa kuhakiki vielelezo kutokuwapo.


Lulu anakabiliwa na shtaka la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu na amekuwa akishikiliwa katika mahabusu ya Gereza la Segerea tangu Aprili mwaka jana.

Akitoa uamuzi wa dhamana jana, Jaji Zainabu Muruke aliyesikiliza maombi hayo alisema msanii huyo ataachiwa huru baada ya masharti hayo kuhakikiwa na Msajili wa Mahakama.
“Mleta maombi anashtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, ambalo lina dhamana, tofauti na kosa la kuua kwa kukusudia. Hivyo, dhamana ni haki ya msingi ya mleta maombi,” alisema Jaji Muruke wakati akisoma uamuzi wake na kuongeza:

“Jamhuri kwa kutambua hilo wamesema hawana pingamizi kwa maombi ya dhamana yaliyoletwa na mawakili wa mleta maombi, hii si kwa matakwa yao bali ni kwa sababu ya sheria.”Akijibu maombi ya wakili mwingine wa msani huyo, Fulgence Masawe kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kulegeza masharti ya dhamana, Jaji Muruke alisema:

“Licha ya kuwa dhamana ni haki ya msingi lakini tukubaliane kuwa pia kuna roho ya mtu imepotea. Hivyo taratibu za kisheria lazima zifuatwe. Hata hivyo, sheria iko wazi kuwa dhamana ni haki ya mleta maombi.”

Masharti yaliyotolewa ni kuwasilisha hati ya kusafiria kwa Msajili na kutosafiri nje ya Dar es Salaam bila idhini ya msajili wa mahakama.

Masharti mengine ni kuripoti kwa Msajili wa Mahakama hiyo kila tarehe moja ya mwezi hadi kesi yake ya msingi itakapomalizika na kuwa na wadhamini wawili ambao wanafanya kazi serikalini watakaosaini bondi ya Sh20 milioni kila mmoja.
Jaji Muruke alisema kabla ya kuachiwa huru, ni lazima Msajili wa Mahakama ahakikishe kuwa masharti hayo yametekelezwa.

Mmoja wa mawakili wake wanaomtetea, Peter Kibatala alisema walikuwa tayari kutekeleza masharti yote yaliyotolewa na mahakama hiyo, lakini walishindwa kutokana na msajili kutokuwapo mahakamani ikielezwa kwamba alikuwa nje kwa kazi nyingine za kimahakama.

“Kwa upande wetu tunaamini kuwa tumetimiza masharti yote sasa hatujui kwa upande wa msajili mwenyewe ambaye ndiye anapaswa kuyahakiki,” alisema Wakili Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kuongeza:

“Tunazo nyaraka zote zinazohitajika pamoja na wadhamini wote wawili ambao wako tayari kusaini hiyo bondi ya Sh20 milioni kila mmoja. Wote wanafanya kazi serikalini, mmoja ni daktari na mwingine yuko Wizara ya Ardhi, lakini tumeshindwa kwa sababu msajili hayupo.”
Kabla ya Mahakama kutoa uamuzi wake wa kukubali maombi hayo ya dhamana, Wakili Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa wamewasilisha maombi hayo ya dhamana chini ya Kifungu cha 148 (10 na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Mawakili wa Serikali, Joseph Maugo na Kishenyi Mutalemwa walisema Jamhuri haina pingamizi dhidi ya maombi hayo, lakini akaiomba Mahakama katika kutoa uamuzi wa dhamana, izingatie Kifungu cha 148 (6) cha CPA juu ya masharti ya dhamana.

Awali, kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali ukiwamo upelelezi, huku akikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia kinyume cha kifungu cha 196.

No comments: