Friday, July 12, 2013

Alex Massawe mbaroni Dubai

Alex Massawe


Mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Massawe ambaye alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu, amekatwa Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) limeripoti gazeti la Mwananchi
Mkuu wa la Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile aliliambia gazeti la Mwananchi jana kwamba Massawe alikamatwa kati ya Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.
Babile alisema hivi sasa walikuwa wanaandaa taratibu za kumrudisha nchini ambako amekuwa akisakwa kwa muda mrefu.
“Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request), lina hatua ndefu. Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza ili Massawe aletwe. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Alisema Massawe alikamatwa wakati akifanya taratibu za ukaguzi baada ya kuwasili UAE.
Habari zilizofikia gazeti la Mwananchi mapema kutoka Dubai zilieleza kuwa Massawe alikamatwa na maofisa wa usalama wa UAE kutokana na alama zake za vidole na kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya watu waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Massawe ambaye anamiliki majumba na biashara ya utalii katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe.
“Maofisa wa Usalama wa uwanja wa ndege walimuuliza kuwa wewe ndiye Alex Massawe? Alikana lakini alielezwa kuwa alama za vidole vinaonyesha anaitwa hivyo,” kilidokeza chanzo cha habari hizi kwa simu kutoka Dubai. Hata hivyo, Babile alisema hakuwa na taarifa za Massawe kukutwa na pasi bandia za kusafiria.
Uvumi wa Aprili
Mapema Aprili 27, mwaka huu kulikuwa na habari kwamba Massawe amekamatwa katika mji mmojawapo ulioko katika Pwani ya Afrika Kusini.
Habari hizo za kukamatwa kwa Massawe, ambaye pia hufadhili masuala ya kisiasa na michezo, zilisambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya Facebook, Twitter na Jamii Forum. Kulikuwa kuna mkanganyiko wa taarifa huku wengine wakidai alinaswa akiwa ndani ya boti huko Afrika Kusini, wengine wakidai alikamatwa wakati akijaribu kuingia Msumbiji akitokea Malawi.
Akizungumzia hilo Babile alisema huo ulikuwa ni uzushi na baada ya kuzisikia taarifa hizo walifuatilia katika maeneo aliyohusishwa kukamatwa na kubaini kwamba hapakuwa na ukweli wowote.
Kwa nini Massawe anatafutwa
Aprili 4 mwaka huu, mfanyabiashara huyo alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’ na mshtakiwa mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja. 
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe akamatwe.
Source: Mwananchi