Thursday, October 25, 2012

JWTZ yasema Malawi haijarusha Mabomu Mpaka upo salama

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania  (JWTZ )Col. Kapambala Mgawe
 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema mpaka wa Tanzania na Malawi ni salama, hivyo hakuna sababu kwa wananchi kuingiwa na hofu kwa kuwa jeshi lipo eneo hilo kuimarisha ulinzi.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema hayo jana wakati akihojiwa na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One, kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa kuna mabomu yamerushwa upande wa Tanzania toka nchi jirani ya Malawi.

“Hali ya mpakani  ni shwari na jeshi liko huko, kama hali ingekuwa mbaya tayari Mbeya ingekuwa imehamwa, wananchi wasiwe na wasiwasi kabisa hakuna mabomu yeyote yaliyorushwa,” alisema Mgawe.

Alisema taarifa zilizosambazwa kwamba kuna mabomu yamerushwa toka Malawi ni jambo ambalo  limetengenezwa ili kuwatia hofu wananchi kwasababu tu kulikuwa na kutofautiana kati ya Tanzania na Malawi. Alisema suala hilo kwa sasa linashughulikiwa na viongozi wa nchi hizo kwa njia ya mazungumzo.

“Sidhani kama Malawi wanaweza wakafikia hatua ya kurusha mabomu, taarifa hizi ni za uzushi, hata namba zilizoandikwa  siyo za jeshi ni mtu ametunga tu,”alisema Mgawe.

Mgawe alisema hata hivyo JWTZ lipo katika harakati za  kufanya utafiti kubaini mmiliki wa namba iliyotumika kusambaza ujumbe huo na kwamba pia inawezekana watu wakafanya hivyo kwa ajili ya kufanya biashara zao.

Kuhusu ushirikiano kati ya JWTZ na makampuni ya simu, alisema watawasiliana na wenye mitandao ya simu na kwamba hata hivyo wananchi wasiogope na kujenga hofu katika jambo ambalo siyo la ukweli na badala yake waendelee na shughuli zao kama kawaida.

No comments: