Tuesday, October 2, 2012

Vigogo waendelea kula mweleka CCM

Baada ya Sumaye sasa Bregedia Ngwilizi naye  chali


Sumaye aahidi kupasua jibu yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi


NAIBU Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, ameshindwa nafasi ya kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kupitia Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga.

Ngwilizi, ambaye pia ni Mbunge wa Mlalo, alipigwa mweleka katika uchaguzi huo na Mfanyabiashara Najim Msenga, aliyemshinda kwa kura 895, dhidi ya 651 alizopigiwa Ngwilizi.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum, Ummy Mwalimu.

Katika matokeo mengine, Balozi Abdi Mshangama alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Lushoto, baada ya kupigiwa kura 1,098 na kuwashinda Mathew Mbarouk aliyepigiwa kura 733 na Sufiani Shekolowa aliyepata kura 76.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Magid Mwanga, alishinda nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kwa kupata kura 1,211.

Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, aliibuka mshindi katika nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kupitia Wilaya ya Monduli.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana, Lowassa alipata kura 709, huku Nanai akiambulia kura 44 na Dk. Salashi Toure akiambulia kura 7.

Dalili za Lowassa kushinda zilionekana kabla ya kupigwa kura, ambapo mpinzani wake, Dk. Salash Toure alikuwa na hali mbaya kutokana na kuzomewa kila wakati na kutakiwa kuondoka mbele ya wapiga kura.

Baada ya kuona hali ni tete mbele ya wajumbe, Dk. Toure aliamua kutangaza kujitoa na kumuunga mkono mgombea Nanai Konina.

Akiomba kura kwa wajumbe waliokuwa wakipiga vigelegele muda wote, Lowassa alipewa dakika 3 za kujinadi na kuomba kura, lakini hakutumia muda wote huo.

“Ndugu zangu, leo historia inajirudia, Monduli Oyeeeee, macho na dunia yote yakiwamo ya Watanzania, yapo hapa kuangalia mtanifanyia nini katika uchaguzi huu wa leo.

“Anaweza akauliza mtu, nategemea dakika zangu zinahesabiwa, Monduli Oyeeeee, nisikilizeni dakika zangu zinaweza kuisha bure kabla sijasema. Anaweza kukuuliza mtu, kwa nini ninagombea, mwambie kwa jeuri na uhakika, ninagombea kwa sababu sasa hivi Monduli ina amani tuliyoitengeneza vizuri.

“Miaka michache iliyopita, ilikuwa ukija kutoka Arusha barabara ya lami inaishia Kosovo, leo tuna barabara ya lami mpaka Monduli Juu. Tulikuwa na matatizo makubwa ya maji tumeyapunguza kwa kiwango kikubwa, hali ni nzuri,” alisema Lowassa.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili kwa sasa, alibainisha kwamba wanaendelea na juhudi za kuyapunguza matatizo katika maeneo kadhaa, yakiwamo ya Lepurko na Mbuyuni. Alisema kwa upande wa eneo la Nararami na maeneo mengine tayari juhudi zinafanyika za kumaliza changamoto zinazowakabili kabla ya muda wao wa uongozi kwisha.

“Katika sekta ya afya, tumefanya vizuri, Monduli Oyeeeee, kwani kwenye akaunti ya Mkurugenzi wa Halmashauri tuna Sh milioni 850 zitakazotumika kujenga hospitali mpya ya wilaya yetu kama nilivyoahidi.

“Lakini kana kwamba haitoshi, kata 10 tumejipanga kuzijengea zahanati mpya, tukijielekeza kwenye elimu, ni wazi kuwa leo wilaya ya Monduli ni moja ya wilaya za mbele katika kutekeleza suala la elimu nchini.

“Sasa naomba kwa heshima na taadhima, umshike jirani yako mkono na umwambie mpe Lowassa kura,” alisema Lowassa huku kelele za shangwe zikitawala ukumbi huo.

Dk. Toure aliyeingia ukumbini akiwa tayari amekuta hali ya hewa imechafuka, huku akiwa na hotuba yake mkononi, alianza kwa kuwasalimia wapiga kura ambao nao walianza kumtaka aondoke mbele yao.

“Kwa heshima na taadhima namshukuru Mola wetu kwa kutuwezesha kukutana hapa kimwili na kiakili, ndugu zangu mkiwa wawakilishi wa wananchi katika maeneo yenu, mmepewa dhamana kubwa ya kuchagua viongozi watakaokuwa hatua kubwa ya maendeleo ya Monduli.

“Nimesimama mbele yenu kutaka kugombea kiti hicho ‘nafasi hiyo’, nimesimama kwa sababu ya mengi tu, wengine watakubaliana nami wengine watakataa. Bado natofautiana na maendeleo yaliyopo wilayani Monduli sana tu.”

Hata hivyo baada ya hali kuwa tete zaidi kutokana na ukumbi kumzomea na kumtaka aondoke mbele yao, ndipo Dk. Toure alipoonekana kuacha kuendelea kusoma hotuba yake na kuwaangalia wajumbe hao.

“Napenda kusema hivi kutokana na udugu wetu, mwana wetu aliye pamoja na sisi anayeitwa Nanai, mimi Dk. Toure nasema hivi namwachia nafasi hiyo, nimeamua kujitoa kwa ajili yake. Ninaomba kura kwa ajili ya nani?"

Naye Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Monduli, Reuben ole Kunai, alifanikiwa kutetea nafasi yake.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi, wasiugeuze uchaguzi kuwa ni suala la kufa na kupona. Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wagombea hao wasiwe na kinyongo baada ya uchaguzi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana ilisema kuwa, Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Katavi, kwenye mkutano uliofanyika Shule ya Sekondari ya Milala, iliyopo wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi.

“Tunapoomba nafasi hizi tusiligeuze suala hili kuwa ni la kufa na kupona, hivi huko tunakotaka kwenda kuna nini? Ni kwa nini tunawekeana kinyongo baada ya uchaguzi wakati hii ni nafasi tu ya kuwahudumia wana CCM wenzio?” alihoji Waziri Mkuu na kushangiliwa.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM, aliwataka wagombea wa nafasi hizo wawe tayari kupokea matokeo kwa moyo mkunjufu na kuvunja makundi baada ya uchaguzi kukamilika.

Katika uchaguzi huo, Wilaya za Mpanda ziligawanywa kwa mara ya kwanza kutokana na kuundwa kwa mkoa mpya wa Katavi.

Katika mazungumzo yake, Waziri Mkuu Pinda, aliwataka viongozi watakaoteuliwa wawe wanafuatilia kwa makini utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kudai taarifa za maendeleo kutoka kwa watendaji wa vijiji na kata kila baada ya miezi mitatu.

“Katibu wa tawi una wajibu wa kumwandikia barua Ofisa Mtendaji wa Kijiji na kudai taarifa za miezi mitatu na taarifa hizo zionyeshe mapato na matumizi. Asipofanya hivyo, unamwandikia barua ya kumkumbusha, asipotekeleza, peleka taarifa ngazi ya juu nasi tukipewa taarifa, tutashughulikia na naamini tukitimua wawili watatu hivi, heshima ya kazi itarudi,” alisema.

Katika uchaguzi uliofanyika kuanzia jana mchana hadi usiku wa manane na matokeo yake kupatikana saa 9 alfajiri, Philip Kalyalya, alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mlele kwa kupata kura 500 na kuwabwaga wapinzani wake, Jacob Mambosasa aliyepata kura 111 na Joseph Msabaha aliyepata kura 100.

Katika nafasi za ujumbe wa NEC Taifa, Thomas Kampala aliibuka mshindi kwa kupata kura 436 na kumbwaga mpinzani wake, Jacob Msyete aliyepata kura 250.

Nafasi za wajumbe watano wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa zilinyakuliwa na Winfrida Katabi aliyepata kura 420, Nyasongo Serengeti alipata kura 357, Emmanuel Pondamali, kura 305, Pascal Sanane, kura 262 na Augustino Mbalamwezi aliambulia kura 237.

Kwa upande wa Wilaya ya Mpanda, Beda Katani, alishinda kwa kupata kura 472 na kufuatiwa na Fulgensia Kapama aliyepata kura 208. Kwenye ujumbe wa NEC Taifa, Suleiman Kakoso aliibuka mshindi kwa kupata kura 352 na kuwashinda Pius Bizumale aliyepata kura 235 na Gabriel Mnyele alipata kura 85.

Wajumbe watano walioshinda nafasi za Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na kura zao kwenye mabano ni Sebastian Kapufi (512), William Mbogo (424), Michael Kapata (275), Ramadhan Kala (242) na Yasini Katampa (206).

No comments: