Wednesday, November 7, 2012

Kikwete aungana na marais duniani kumpongeza Obama

Rais Kikwete katikati akiwa na Rais Barak Obama pamoja na mkewe Michelle Obama

Rais Obama akimkaribisha White House Rais Kikwete alipokwenda kumtembelea na kuvunja rekodi kuwa rais wa kwanza barani Afrika kukutana na Rais Barak Obama

Rais Kikwete na Obama wakatika mazungumzo wakati walipomtembelea Obama nchini Marekani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza furaha na shangwe yake kufuatia ushindi wa jana, Jumanne, Novemba 6, 2012 wa Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu katika salamu za pongezi kwa kiongozi huyo wa Marekani ambaye amechaguliwa tena na wananchi wa nchi hiyo kwa kipindi cha pili, Rais Kikwete amesema
 “Nimepokea kwa furaha na shangwe habari za kuchaguliwa tena kwako kuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha pili. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe na kupitia kwako Chama cha Democratic pongezi nyingi kwa ushindi wako wa maana sana.”

Ameongeza Rais kikwete katika salamu zake hizo: “Kuchaguliwa kwako tena kuendelea kuongoza nchi yako muhimu na wananchi wake, ni ishara ya wazi ya uaminifu na imani ambayo wananchi wa Marekani wanayo katika uongozi wako wa mfano.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati unajiandaa kuchukua tena uongozi wa nchi hiyo katika kipindi chako kipya, napenda kukuhakikishia msimamo wangu binafsi na ule wa Serikali yangu kuwa tutaendelea kufanya kazi kwa karibu kabisa na wewe na Serikali yako ya kutukuka, ili kuendeleza uhusiano bora ulioko kati ya nchi zetu mbili ndugu.”