Sunday, March 24, 2013

CHADEMA wapanga kuandamana kumng'oa Waziri wa Elimu


Wakati wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakipanga kufanya maandamano makubwa leo jijini Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ajiuzulu, Jeshi la Polisi limewapiga marufuku kwa maelezo kuwa maandamano hayo ni batili.
Takriban wiki mbili zilizopita viongozi wa chama hicho katika mikoa hiyo, kwa nyakati tofauti walitangaza kufanyika kwa maandamano hayo, lengo likiwa ni kushinikiza Dk Kawambwa na naibu wake, Philipo Mulugo kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya watahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana.

Wakati polisi wakizuia maandamano hayo kwa maelezo kuwa Serikali imeshaunda tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome, kuchunguza chanzo cha kufeli kwa asilimia 65 kwa watahiniwa hao, Chadema wamesema lazima maandamano yafanyike na wako tayari kufa.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesisitiza kuwa maandamano ya kumshinikiza Dk Kawambwa kujiuzulu yatafanyika kesho kama yalivyopangwa licha ya Jeshi la Polisi kuyapiga marufuku.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mbowe alisema iwapo Serikali itaamua kutumia risasi na mabomu kuua raia wake wanaoandamana kwa amani kuonyesha hisia ya kuchukizwa na matokeo mabaya ya kidato cha nne, basi itimize dhamira hiyo kwa kuwapiga risasi waandamanaji.
“Kama CCM na serikali yake itatumia risasi na mabomu kuua watu kumlinda waziri mmoja asijiuzulu, basi wafanye hivyo. Sisi tutaandamana kama tulivyotangaza mwezi mmoja uliopita na tunaomba dunia ielewe hivyo,” alisema Mbowe.
Alisema wameamua kuendelea na maandamano hayo baada ya kutoridhishwa na sababu zilizotolewa na polisi kuzuia maandamano hayo, ikiwamo ile ya CCM kudaiwa kuandaa maandamano siku hiyohiyo kupitia njia zilezile zilizotajwa na Chadema.
Mbowe alisema maandamano hayo yatafanyika katika majiji manne ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam na kuwataka wananchi wanaoishi jirani na miji hiyo kujitokeza kwa wingi kuandamana kwa mustakabali wa watoto wao wasiopata elimu bora kama wapatayo wale wa viongozi.
Chadema Mkoa wa Dar
Katibu wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam, Henry Chilewo akizungumza na vyombo vya habari jana alisema, maandamano hayo yatahusisha wananchi wa kada zote.
“Mwenyekiti wetu (Freeman Mbowe) alitoa siku 14 kwa viongozi hao wajiuzulu kwa hiyari lakini wamegoma, tunaamini nguvu ya umma wa Watanzania itafanikisha hilo na ifahamike wazi kuwa lengo letu ni kudai elimu bora kwa watoto wetu,” alieleza Chilewo.
Kauli ya Kamanda Kova
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliliambia gazeti hili kwamba bado jeshi hilo linafanya tathmini kabla ya kutoa kauli ya mwisho.
“Bado tunafanya tathmini, kesho (leo) tutaeleza kama yatakuwapo au hayatakuwapo,” alisema Kova.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Temeke, Englebert Kiondo alisema maandamano hayo ni batili kwa sababu tume imeshaundwa.
“Kesho (leo) Rais wa China, Xi Jingping anakuja nchini hivyo si vizuri akafika na kukutana na maandamano, nawaomba wananchi wa Temeke wasishiriki katika maandamano haya, waendelee na shughuli nyingine,” alisema Kiondo.

Source: Mwananchi

No comments: