Wednesday, July 6, 2011

Pinda azungumzia masuala ya uharamia

Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda
 
WAZIRI MKUU wa Tanzania Mizengo Pinda amesema suala la uharamia linahitaji kupata nguvu zaidi ya kukabiliana nalo kutoka ngazi ya Umoja wa Afrika (AU) na lisichukuliwe kuwa ni jambo linaloweza kutatuliwa na Serikali ya Tanzania peke yake.
 
Ametoa kauli hiyo janai (Jumanne, Julai 05, 2011) nyumbani kwake, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Mjumbe Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia anayeshughulikia masuala ya Dharura na Mazingira Hatarishi kwa Binadamu (Special Envoy of the Italian Minister for Foreign Affairs on Humanitarian Emergencies and Vulnerable Situations), Bibi Margherita Boniver.
 
“Suala la uharamia si suala la Tanzania au nchi za Afrika Mashariki peke yake bali umeshakuwa mgogoro wa kimataifa (international crisis) unaohitaji kuangaliwa kwa mapana yake ili kupata suluhu ya kudumu.”
 
Waziri Mkuu Pinda alisema kwamba suala la uharamia linaloendelea hivi sasa kuanzia Pwani ya Pembe hadi nchi za Afrika Mashariki linaziathiri nchi nyingi na siyo Tanzania peke yake kwa hiyo inabidi liwasilishwe katika ngazi ya Umoja wa Afrika ili lipate msukumo wa nguvu zaidi.
 
“Mwaka 2008 kulikuwa na matukio 146 ya utekaji nyara, mwaka 2009 yakafikia 160 na mwaka 2010 matukio yalikuwa 26. Mwaka jana matukio yalipungua kutokana na juhudi ambazo Serikali ilichukua ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria na kutoa mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema.
 
“Ukiangalia matukio hayo yote utaona kuwa idadi hii si ndogo hata kidogo, na inatuumiza kiuchumi kwani wote kama wadau tunauhitaji mfereji wa Suez kupitisha bidhaa zetu kwa vile ni njia fupi ya kufika Ulaya ukilinganisha na ya kuzungukia Afrika Kusini ambayo ni ya gharama zaidi,” aliongeza.
 
Akizungumza katika kikao hicho, Bibi Boniver ambaye pia ni mbunge huko Italia alisema suala ya uharamia limewaathiri sana kwani hasi sasa kuna meli mbili za Italia zilizokamatwa na zikiwa idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo ambao bado wanashikiliwa na maharamia hao. Hata hivyo, hakutaja idadi ya raia ambao wanashikiliwa hadi sasa.
 
“Meli zetu mbili zilikamatwa Februari na Aprili mwaka huu… kuna watu wetu wako huko ambao bado wanashikiliwa na maharamia… tunajua wako hai lakini tunahisi watakuwa na hali mbaya,” alisema Mjumbe huyo ambaye alikuwa na ziara fupi hapa nchini kwa shughuli hiyo maalumu ya kuomba Serikali ya Tanzania isaidie kuingilia kati suala la raia wa Italia waliotekwa na maharamia.
 
Alisema Tanzania na Italia zinafanana kijiografia katika suala la kukabiliana na maharamia kwani zinakabiliwa na changamoto inayofanana kutokana na fukwe ndefu ilizonazo. “Hii ni changamoto kwetu sote lakini kutokana na uzoefu tulionao, tunaweza kusaidia kutoa mafunzo kwa askari wa Tanzania,” aliongeza.
 
Alisema anakubaliana na kauli ya Waziri Mkuu Pinda kwamba suala la uharamia haliwezi kumalizwa na nchi moja na kukiri kwamba linahitaji juhudi za pamoja za kukabiliana nazo.
 
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Pinda amefanya mazungumzo na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Rosatom ambayo inamilikiwa na Serikali ya Russia na inajihusisha na masuala ya nguvu za nyuklia, Bw. Sergei Kiriyenko ambaye aliongoza ujumbe wa wawekezaji kutoka Russia ambao wanahusika na uchimbaji wa madini ya Uranium nchini Tanzania.
 
Pia Bw. Kiriyenko ameongoza ujumbe huo akiwa ni Mjumbe Maalum wa Rais wa Russia, Bw. Dmitry Medvedev.
 

No comments: