Friday, September 23, 2011

Sata wa upinzani ashinda urais Zambia

Michael Sata

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia Michael Sata amechaguliwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

Sata ametangazwa kuwa mshindi na Jaji Mkuu wa nchi hiyo Ernest Sakala baada ya kupata asilimia 43 huku takribani kura za majimbo saba zikiwa bado hazihesabiwa.

Kutangazwa kwa Sata kunakuja baada ya siku mbili za vurugu katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo na hasa eneo la kaskazini ya nchi hiyo wakati wa zoezi la kuhesabu kura.

Kiongozi huyo wa upinzani kutoka chama cha Patriotic Front anachukua nafasi ya Rais wa sasa Rupia Banda kutoka chama tawala cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) ambaye ameongoza nchi hiyo kwa takribani miaka mitatu baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo marehemu Levy Mwanawasa mwaka 2008.
Awali watu wawili waliuawa kufuatia ghasia katika maeneo ambayo ni ngome ya upinzani.
Mkuu wa Polisi wa jimbo hilo maafuru kwa uzalishaji Shaba ameliambia shirika la habari la Reuters watu wamejitokeza katika barabara za mji wa Kitwe na Ndola wakivurumisha mawe.
Taarifa zinasema ghadhabu hizi zimechochewa na agizo la serikali kupiga marufuku vyombo vya habari kutangaza matokeo bila ya idhini ya tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.

No comments: