Tuesday, October 30, 2012

Bunge laanza: Ripoti ya Wabunge waliohongwa utata


WAKATI Bunge likianza mkutano wake wa Tisa leo, zipo taarifa Ripoti ya Kamati  ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa haitasomwa na kisha kujadiliwa.

Badala yake, kwa mujibu wa watoa habari wetu, Kamati ya Uongozi, iliyokutana jana iliamua kwamba litatolewa tamko kuhusu ripoti ya kamati hiyo, hivyo haitasomwa wala kujadiliwa kama ambavyo wabunge wamekuwa wakitaka.

Kwa maana hiyo Spika wa Bunge, Anne Makinda huenda akatumia kanuni nyingine kutoa tamko kuhusu uchunguzi huo, hali ambayo haitatoa fursa kwa wabunge kuijadili kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakishinikiza.



Miongoni mwa kanuni ambazo Spika anaweza kuzitumia ni pamoja na ile ya 33 (2) ambayo inasema: “Wakati wa kikao, Spika anaweza kutoa taarifa nyinginezo kadri atakavyoona inafaa.”

Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel jana alikataa kuzungumzia suala hilo akiahidi kulitoa ufafanuzi leo... “Ratiba ya shughuli za Bunge bado iko kwenye ngazi ya Kamati ya Uongozi. Sasa pengine tusubiri kesho (leo) ikiwa tayari kila kitu kitakuwa wazi, hakuna haja ya kuwa na haraka.”

Jana, Kamati ya Uongozi wa Bunge ilikutana mjini Dodoma kujadili mambo mbalimbali na habari zinasema kwamba suala la Ripoti hiyo ya Ngwilizi, pia lilijadiliwa.

Agosti 2 mwaka huu, Spika Makinda aliunda kamati hiyo ndogo kuchunguza tuhuma za rushwa zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya wabunge ambao walidaiwa kwamba walihongwa ili kuikwamisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Kuundwa kwa kamati hiyo, kulitanguliwa na tukio la kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Julai 28, mwaka huu pia kutokana na tuhuma hizohizo.

Tayari kumekuwa na taarifa kwamba ripoti hiyo imevuja na maudhui yake kuchapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari, hali ambayo ilisababisha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuonya kwamba waliohusika na kuvuja huko huenda wakajikuta matatani kwani ni kosa la kisheria.

“Kitendo cha kuchambua na kuchapisha maudhui ya taarifa hiyo katika vyombo vya habari ni kinyume cha sheria na kinaingilia uhuru, haki na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 31 (1) (g) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura 296,” alisema Ndugai katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni.

Mmoja wa wabunge ndani ya kamati iliyochunguza suala hilo (jina tunalihifadhi kwa sasa), ndiye anayedaiwa kwamba aliivujisha ripoti hiyo ya uchunguzi kwa makusudi, lengo likiwa ni kumshinikiza Spika Makinda aitoe hadharani ili kuwasafisha watuhumiwa.

Mbunge huyo alifanya hivyo kwa msukumo wa baadhi ya wabunge waliotuhumiwa kujihusisha na rushwa, pamoja na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kabla ya kuvunjwa.
Kadhalika, Ndugai katika mkutano wake na vyombo vya habari alisema suala la ripoti hiyo kusomwa bungeni au vinginevyo linategemea uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Ndugai alisema baada ya kamati kuwasilisha ripoti kwa Spika, Kamati ya Uongozi ya Bunge itakaa kujadili na kama itaona kuna umuhimu wa kuingizwa katika ratiba ya vikao vya Bunge ijadiliwe.

Alisema Vifungu 114 (17) na 119 (1) hadi (6) vya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007 kwa pamoja vinampa madaraka Spika kuhusu utaratibu wa kufuata katika uwasilishaji wa taarifa bungeni.

Kamati hiyo iliyoundwa na Spika ilikuwa chini ya Ngwilizi ambaye ni Mbunge wa Mlalo, ina wajumbe; Said Arfi (Mpanda Kati), John Chiligati (Manyoni Mashariki), Goesbert Blandes (Karagwe) na Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Omary Juma. Kamati hiyo ilimaliza kazi yake na kuiwasilisha kwa spika tangu Septemba 20 mwaka huu.

Source: Gazeti la Mwananchi

No comments: