Sunday, November 4, 2012

Pangua Makamanda wa Polisi: CHADEMA wauliza kwanini RPC Iringa abaki?

IGP Said Mwema (kushoto) na kulia Polisi wakimshughulikia Mwandishi wa habari Marehemu Daudi Mwangosi ambaye baadae alilipuliwa na bomu


KURUGENZI ya Ulinzi na Usalama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imesema uteuzi uliofanywa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, umedhihirisha wazi Polisi haina dhamira ya dhati ya kuhakikisha haki inatendeka kwa watu wote, na kusisitiza uwajibikaji, ikiwa moja ya misingi muhimu kwa amani na utulivu wa nchi.
IGP Mwema, juzi alifanya mabadiliko kwa baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa na vikosi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ulinzi wa Usalama CHADEMA, Wilfred Lwakatare, alisema kuwa, inashangaza kuona panga pangua hiyo iliyofanywa na IGP Mwema imeshindwa kuona ukweli na kuzingatia maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa inawaondoa makanda wote waliokumbwa na kashfa za mauaji.

Lwakatare alisema kuwa, kupitia taarifa hii, wataendelea kusisitiza azimio la Kamati Kuu ya chama hicho pamoja na barua iliyoandikwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, kumwajibisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, IGP Mwema, Kamishina Chagonja, RPC Shilogile, RPC Kamuhanda na Kamanda wa FFU Mkoa wa Morogoro, kutokana na mauaji yaliyotokea Morogoro na Iringa.

“Kwa namna yoyote ile, katika wakati kama huu ambapo vyombo vya dola, likiwemo Jeshi la Polisi, vikiandamwa na tuhuma kali zinazohusisha matukio ya kuteka, kutesa na kuua raia, ambao ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, katiba na sheria za nchi, ilitegemewa panga pangua yoyote iendane na watuhumiwa wote wa matukio hayo kuwajibika,” alisema.

Lwakatare alisema kuwa, IGP Mwema bila kuzingatia ukweli kuwa jeshi hilo analoliongoza liko katikati ya tuhuma za mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, hivyo hatua ya kufanya uteuzi wowote usiozingatia ukweli huo, hauwezi kuondoa doa kubwa linaloandama jeshi hilo mbele ya macho ya Watanzania.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: